
100 episodes

Habari za UN - Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu United Nations
-
- News
-
-
5.0 • 5 Ratings
-
Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
-
Sitisha uhasama miongoni mwa wakimbizi wa ndani Sudan Kusini: UNMISS
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS umetoa wito wa kusitishwa mara moja kwa uhasama miongoni mwa wakimbizi wa ndani katika Kambi ya Umoja wa Mataifa ya Ulinzi wa Raia nchini humo kufuatia tukio la jana Alhamis ambapo watu kadhaa waliripotiwa kujeruhiwa na wengine kuuawa.
Video iliyorekodiwa na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) inaonesha gari la wagonjwa la Umoja wa Mataifa likisindikizwa na walinda amani likipita katika barabara ya vumbi katikati ya umati wa wakimbizi wa ndani katika eneo la Malakal nchini Sudan Kusini.
Kila mmoja aliyefanikiwa kusalia na chochote katika anavyovimiliki, amekibebeba kichwani, mgongoni au mkononi.
Jana muda wa mchana ghasia zilizuka kati ya jamii mbili za wakimbizi wa ndani ambazo zimehifadhiwa katika Kambi ya Umoja wa Mataifa ya Ulinzi wa Raia.
UNMISS inasema vurugu hizo zilichochewa na tukio la kuchomana visu huku ripoti za awali zikitaja raia watatu kuuawa na wengine 20 kujeruhiwa hadi kufikia jana Alhamisi mchana.
Kabla ya hapo, hiyo-hiyo jana Alhamis asubuhi, milio ya risasi ilitanda alfajiri katika mji mkuu wa jimbo la Upper Nile, Malakal, karibu na makazi ya UNMISS.
Walinda amani wa UNMISS waliingia kazini haraka kwa kuwa hali ya wasiwasi imekuwa ikiendelea hapa tangu mwisho wa wiki iliyopita, wakati mzozo katika kituo cha maji uliongezeka haraka na kuwa mzozo kamili ambapo mtu mmoja mwenye umri wa miaka 32 aliuawa.
Kwa kuwa kambi ya walinda amani iko karibu na kambi ya Umoja wa Mataifa ya ulinzi kwa raia, mara zote walinda amani wako chonjo kuchukua hatua ya haraka pindi tu wanapopokea taarifa ya vurugu.
Wakati wa mapigano ya mwezi uliopita, wanajeshi na polisi walinda amani walitumwa mara moja ili kutuliza hali hiyo.
Polisi na walinda amani wa kijeshi kwa sasa wanashika doria ndani ya eneo hilo na kuzunguka eneo la nje, kwa ushirikiano na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Sudan Kusini ili kuondoa hofu miongoni mwa jamii iliyokimbia makazi yao.
Zaidi ya hayo, walinda amani matabibu katika hospitali ya UNMISS wanatoa huduma ya dharura kwa baadhi ya waliojeruhiwa.
Kwa mujibu wa usajili wa kibayometriki wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM), kufikia Desemba mwaka jana 2022, baadhi ya watu 37,032 waliokimbia makazi yao wanajihifadhi katika Eneo la Ulinzi la Umoja wa Mataifa la Malakal. -
OHCHR yapokea ripoti za raia kuuawa na wanawake kubakwa nchini Sudan
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binaadamu, OHCHR imeeleza kusikitishwa na athari mbaya za mapigano kwa raia zinazoendelea nchini Sudan ambapo mpaka hizi sasa wamepokea taarifa za kuuawa kwa raia ikiwemo watoto na wajawazito na ubakaji huku waandishi wa habari wakiwa katika hali mbaya kutokana na kauli za chuki hususani mitandaoni.
Akizungumza na waandishi wa habari hii leo jijini Geneva Uswisi msemaji wa Ofisi hiyo ya Haki za Binadamu Jeremy Laurence amesema,
“Kwa wiki hii pekee limetokea shambulio katika soko la mifugo lenye shughuli nyingi katika mji mkuu Khartoum lilisababisha vifo vya raia wanane, miongoni mwao takriban watatu wanatoka familia moja. Mashambulizi ya anga kwenye soko la Al-Muwaliyyah tarehe 7 Juni yalidaiwa kutekelezwa na Jeshi la Sudan.”
Jeremy pia amezungumzia tukio la mtoto kuuawa akiwa nyumbani kwao na pia uwepo wa ripoti za unyanyasaji wa kingono.
“Tangu mapigano yalipoanza, Ofisi yetu imepokea ripoti za kuaminika za matukio 12 ya unyanyasaji wa kingono yanayohusiana na mzozo huo, dhidi ya angalau wanawake 37, ingawa idadi inaweza kuwa kubwa zaidi. Katika angalau matukio matatu, waathirika walikuwa wasichana wadogo. Katika kisa kimoja, wanawake 18 hadi 20 waliripotiwa kubakwa.”
Ripoti za watu kutoweka na waandishi wa habari kukabiliwa na ongezeko la matamshi ya chuki mitandaoni pia zimeripotiwa. -
09 JUNI 2023
Hii leo jaridani tunaangazia mizozo nchini Sudan ka pia nchi jirani Sudan Kusini. Makala tunakupeleka nchini Somalai na mashinani nchini Tanzania, kulikoni?
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binaadamu, OHCHR imeeleza kusikitishwa na athari mbaya za mapigano kwa raia zinazoendelea nchini Sudan ambapo mpaka hizi sasa wamepokea taarifa za kuuawa kwa raia ikiwemo watoto na wajawazito na ubakaji huku waandishi wa habari wakiwa katika hali mbaya kutokana na kauli za chuki hususani mitandaoni.Na tukitokea huko Sudan tuelekee katika nchi jirani, Sudan Kusini. Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS umetoa wito wa kusitishwa mara moja kwa uhasama miongoni mwa wakimbizi wa ndani katika Kambi ya Umoja wa Mataifa ya Ulinzi wa Raia nchini humo kufuatia tukio la jana Alhamis ambapo watu kadhaa waliripotiwa kujeruhiwa na wengine kuuawa.Makala ambayo leo inatupeleka katika majimbo ya Hijraan na Galmudug nchini Somalia yaliyoathirika vibaya na ukame ulioleta changamoto ya maji kwa wakulima na wafugaji, lakini sasa asante kwa shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO mradi wake wa maji unaleta nuru.Na katika tunakupeleka nchini Tanzania kusikia ni kwa jinsi gani mashirika ya Umoja wa Mataifa wanashirikiana na wadau wake kupambana na magonjwa ya kuambukiza.Mwenyeji wako ni Anold Kayanda, Karibu! -
Asante FAO kwa kutunusuru na ukame: Wafugaji Somalia
Somalia ambayo imekuwa katika machafuko kwa miongo zaidi ya mitatu sasa inaendelea kukabiliana na janga lingine kubwa la ukame ambao haujawahi kushuhudiwa kwa miaka takriban 40 na kuathiri mamilioni ya watu wakiwemo wakulima na wafugaji wa majimbo ya Hijraan na Galmudug. Katika majimbo hayo jamii zimepoteza karibu kila kitu kutokana na ukame huo na kupoteza matumaini. Lakini sasa asante kwa shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO kurejesha matumaini ya jamii hizo kwa kuzindua mradi wa maji ambao sio tuu utazinusuru jamii hizo na mifugo yao lakini pia utazipa matumaini mapya ya maisha. Tuambatane na Flora Nducha katika makala hii kwa ufafanuzi zaidi
-
Jifunze Kiswahili: Uchambuzi wa neno, "RUWI"
Katika kujifunza lugha ya Kiswahili, leo tunafafanuliwa maana ya neno "RUWI" na mtaalam wetu Onni Sigalla, Mhariri mwandamizi wa Baraza la Kiswahili la Taifa nchini Tanzania, BAKITA, Karibu!
-
08 JUNI 2023
Hii leo ni siku mada kwa kina na jaridani tunaangazia siku ya kimataifa ya bahari inayohimiza kuhakikisha bahari inakuwa safi na yenye afya ili iweze kuihudumia vyema jamii tutaangalia namna taka zinazotolewa baharini zinavyoweza kutumika kama malighafi bora ndani ya jamii. Pia tunakuletea habari kwa ufupi zikiwemo …. Na katika kujifunza kiswahili tunabisha hodi kwenye Baraza la Kiswahili la Taifa nchini Tanzania BAKITA kufafanuliwa maana ya neno"RUWI", salía hapo hapo!
Katika siku ya bahari duniani ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akisema bahari ni msingi wa maisha na binadamu tunaitegemea bahari lakini je bahari inaweza kututegemea? Ethiopia inakabiliwa na dharura nyingi huku kukiwa na changamoto kubwa ya ufadhili duni limeonya leo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR na kuongeza kuwa huku kukiwa na watu wapya na wanaoendelea kutawanywa na kuteseka kutokana na ukame, nchi hiyo ya Afrika Mashariki inahaha kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya watu waliokimbia makazi yao nchini kote.Na tukamilishe na habari Njema. Mlipuko wa homa ya Marburg nchini Equatorial Guinea umemalizika leo kwa mujibu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO huku kukiwa hakuna mgonjwa yeyote mpya aliyeripotiwa katika muda wa siku 42 zilizopita baada ya mgonjwa wa mwisho kuruhusiwa kutoka baada ya matibabu. Mlipuko huo, ambao ulitangazwa tarehe 13 Februari, ulikuwa wa kwanza wa aina yake nchini Equatorial Guinea. Jumla ya wagonjwa 17 walithibitishwa na maabara na vifo 12 vilirekodiwa.Na katika kujifunza Kiswahili, leo tunafafanuliwa maana ya neno "RUWI" na mtaalam wetu Onni Sigalla, Mhariri mwandamizi wa Baraza la Kiswahili la Taifa nchini Tanzania, BAKITA.Mwenyeji wako ni Anold Kayanda, Karibu!