Habari za UN - Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari za UN - Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

  1. 17 HR AGO

    Jinsi usawa wa kijinsia na rika katika umiliki wa ardhi unavyochochea ukulima na uhakika wa chakula Kenya

    Mpango wa Usimamizi wa Ardhi (Land Governance program) uliopatiwa jina "Kusaidia kufikia Ajenda 2030 kupitia mageuzi chanya ya ugatuzi wa ardhi (land reforms) katika maeneo ya ardhi za jamii nchini Kenya" umeboresha uhakika wa kupatikana kwa chakula na lishe kupitia upatikanaji wa ardhi kwa wote nchini Kenya. Programu hii imezinduliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kilimo na chakula FAO kwa kushirikiana na Muungano wa Ulaya (EU) katika kaunti 9 ikilenga kuimarisha sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi na umeimarisha usimamizi wa ardhi kwa ajili ya maisha bora na maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika kaunti zote zinazotekeleza. Kupitia video iliyoandaliwa na FAO, Cecily Kariuki anaeleza matokeo yake. Mpango wa Usimamizi wa Ardhi (Land Governance program) uuliopatiwa jina "Kusaidia kufikia Ajenda 2030 kupitia mageuzi chanya ya ugatuzi wa ardhi (land reforms) katika maeneo ya ardhi za jamii nchini Kenya" umeboresha uhakika wa kupatikana kwa chakula na lishe kupitia upatikanaji wa ardhi kwa wote nchini Kenya. Programu hii imezinduliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kilimo na chakula FAO kwa kushirikiana na Muungano wa Ulaya (EU) katika kaunti 9 ikilenga kuimarisha sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi na umeimarisha usimamizi wa ardhi kwa ajili ya maisha bora na maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika kaunti zote zinazotekeleza. Kupitia video iliyoandaliwa na FAO, Selina Jerobon anaeleza matokeo yake katika makala hii..… Wazee wa jamii za kijiji cha Maiyanat iliyoko katika kaunti ya Turkana kaskazini-magharibi mwa Kenya wanafanya kikao cha pamoja hapa, wakiwa wamevalia mavazi yao ya kitamaduni, watoto wakiwa pembeni wakifuatilia kinachoendelea. Wanajadili matumizi mazuri ya mashamba ya jamii zao kwa kuzingatia usawa wa kijinsia na marika yote. Je, awali umiliki wa ardhi ulizingatia usawa huu? Ratinui Macharia ni mwenyekiti wa ardhi ya jamii ya Maiyanat, anasema, “Awali, wanawake na vijana hawakuruhusiwa kushiriki au hata kuchaguliwa kwenye kamati ya ardhi lakini sasa imetuleta sote pamoja.” Lois Kimere ni mwanamke mwanachama wa kamati ya ardhi Maiyanat. “Kulingana na jamii za Maiyanat, wanawake hawakuwa wanaonekana kama watu wenye uwezo wa kuchangia maendeleo ya kijamii. Tulihamasisha wanawake kuhusu mambo ya ardhi, uongozi katika vijijini na katika ngazi za kitaifa hususani serikali, na katika bishara.” Kwa msingi wa dharura, awamu ya kwanza na ya majaribio ya mpango huu ilitekelezwa katika kaunti za Laikipia, Nandi, Pokot magharibi, Baringo, Vihiga, Marsabit, Kajiado, Samburu, Tana River na Turkana. Asha Lekudere ni mwanachama wa ardhi ya jamii ya sereolipi, anasema FAO imeimarisha mtazamo wao. “Zamani tulikuwa na shamba la kikundi. Kisha FAO ikatupeleka kwenye mafunzo kadhaa. Niliweza kujifunza maana ya umiliki wa ardhi kwa jamii yetu ya samburu, uwezo wetu na haki za wanawake.” Chini ya ajenda ya ardhi ya jamii, programu iliwezesha mila shirikishi na jumuishi katika usimamizi wa ardhi kwa njia ya usawa wa jinsia na rika zote. Na hatua gani zinaweza kuchukuliwa mizozo inapotokea? Mpango wa usimamizi wa ardhi umekuza mfumo mbadala wa mahakama, wa kupigania haki za kibinadamu unaojulikana kama AJS, njia bora ya kusuluhisha kesi mashinani na kuachilia ardhi itumike kwa ajili ya jamii zote haraka iwezekanavyo. Jonathan Osewu, Msajili wa ardhi  katika kaunti ya Kajiado anasema, “Katika utamaduni wetu wa kimasai tunazo njia nyingi sana za kutatua mizozo. Kwa hivyo AJS ilipoletwa, ilikuwa ni njia bora ya kuimarisha utaratibu wetu wa jadi wa kutatua kesi.” Na isitoshe, njia za teknolojia za kutoa ramani ya ardhi na rasilimali yote kwa muonekano wa anga, GIS ili kusaidia kufanya maamuzi ya kesi haraka, pia imechangia utangamano katika jamii husika. Vituo hivi vimetekelezwa katika sehemu nyingi ikiwemo kaunti ya Vihiga. Wilber Ottichilo, Gavana wa mkoa wa Vihiga anatoa shukrani kwa FAO. “Kama kaunti ya Vihiga,…

    5 min
  2. 18 HR AGO

    21 NOVEMBA 2024

    Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina inayotupeleka nchini Kenya kushuhudia jinsi mpango wa Usimamizi wa Ardhi uliopatiwa wa "kusaidia jamii kufikia Ajenda 2030” ambao FAO imetekeleza kwa kaunti kadhaa. Pia tunakuletea muhtasari wa habari na uchambuzi wa neno. Hague kwenye mahakama ya kimataifa ya uhalifu inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ICC ambayo leo imetoa kibali cha kukamatwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, Waziri wa zamani wa ulinzi Yoav Galant  na kiongozi wa kundi la kipalestina la Hamas Mohamed Diab Ibrahim al-Masri alimaarufu kama  kwa makosa ya uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhaifu wa vita ulitendeka wakati wa vita inayoendelea baina ya Israel na Hamas.Mjini  Baku nchini Azerbaijan mkutano wa 29 wa mkataba wa nchi wanachanama wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabainchi COP29 unaelekea ukingoni  na leo ukijikita na masuala ya kijinsia na mabadiliko ya tabianchi. Miongoni mwa waliozungumzia changamoto ya tabianchi kwa wanawake ni  Jemimah Njuki, mkuu wa kitengo cha uwezeshaji wa kiuchumi katika shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya wanawake UN Women.“Raia  wanaoshtakiwa katika mahakama za kijeshi nchini Uganda hukosa dhamana sawa ya mchakato wa kisheria kama wale wanaoshtakiwa katika mahakama za kiraia,” amesema Volker Türk, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu hii leo kufuatia tukio la kutekwa kwa mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda Kiiza Besigye akiwa nchini Kenya.Na katika kujifunza lugha ya Kiswahili na hii leo Dkt. Mwanahija Ali Juma, Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili, Zanzibar nchini Tanzania, BAKIZA anafafanua maana ya neno MHARABU”.Mwenyeji wako ni Assumpta Massoi, karibu!

    10 min
  3. 1 DAY AGO

    COP29 Georgina Magesa: Watoto wana haki ya kuishi katika mazingira salama

    Mkutano wa 29 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP29 unaoendelea huko Baku Azerbaijan umeleta pia watoto na vijana wanaharakati wa mazingiria kutoka kote ulimwenguni na kuwapatia fursa kuketi katika meza moja na viongozi ili kuhakikisha mustakabali wao umewekwa katika ajenda ya mkataba huo.  Jukumu lao kama wachechemuzi wa mabadiliko chanya na hitaji la mazungumzo na ushirikiano kati ya vizazi lilitambuliwa rasmi katika matokeo ya Mkutano wa Zama Zijazo, SOTF mnamo Septemba 2024. Georgina Magesa, msichana mwenye umri wa miaka tisa na mwanaharakati wa mazingira, ambaye amewakilisha watoto wenzake kutoka Tanzania katika Mkutano wa 29 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP29 huko Baku, Azerbaijan. Anatoa ujumbe mahsusi akianza kwa kusistiza kuwa watoto pia wana mchango katika kutatua changamoto za mabadiliko ya tabianchi. “Watoto wenzangu duniani kote, nyie pia mnaweza kuleta mabadiliko chanya. Anza na hatua ndogo pia muwe na ndoto kubwa. Panda miti. Hifadhi maji. Jifunze kuhusu mazingira yetu. Kwa Pamoja vitendo vyetu vidogo vitageuka mabadiliko makubwa” Katika mwaka huu wa 2024 ambao viwango vya joto duniani vimevunja rekodi duniani, watoto na vijana wanaendelea kupaza sauti zao wakihimiza viongozi wa dunia kuchukua hatua za haraka zinazohitajika ili kushughulikia janga la mabadiliko ya tabianchi. Georgina anasema Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF liko mstari wa mbele, lakini sasa ni wakati wa mshikamano kwa ajili ya mazingira bora kwa watoto wa leo, na wa zama zijazo.. “Kwa viongozi wa dunia walioko hapa leo, hii si kazi ya UNICEF pekee. UNICEF inafanya kazi nzuri na sisi watoto, lakini tunahitaji msaada wako ili kujenga ulimwengu wa kesho ambapo hakuna mtoto anayepaswa kuchagua kati ya afya na elimu yake; ambapo hakuna mtoto anayekunywa maji yasiyo salama; hakuna mtoto anayekosa shule kwa sababu ya masuala yanayohusiana na mabadiliko ya tabianchi; na ambapo kila mtoto ana nafasi ya kuwa na afya bora na elimu bora.” Georgina anatamatisha kwa kusisitiza kuwa janga la mabadiliko ya tabianchi limenyima watoto haki zao hivyo kwa kila mtu... “Kumbuka unapolinda mazingira unalinda afya, elimu na ndoto za watoto. Mtoto mwenye afya bora na elimu bora anaweza kubadilisha ulimwengu.” Ama kweli watoto wana haki ya kuishi katika mazingira salama!

    4 min
  4. 1 DAY AGO

    20 NOVEMBA 2024

    Hii leo jaridani tunaangazia ripoti siku ya watoto duniani, na kwa kutambua siku hii tunamulika mikutano yote yanayoendelea kwa ajili ya haki za watoto na vijana, ambao wametoa ujumbe wao kutoka Baku nchini Azerbaijan na Denmark wakiwakilisha nchi zao. Leo ni siku ya watoto duniani maudhui mwaka huu yakiwa "Kila mtoto, kila haki"na katika kuhakikisha sauti zao zinasikika kuhusu mustakbali wa utakao, shirika la Umoja wa Maataifa la kuhudumia watoto duniani UNICEF limewapa fursa ya kuandika barua kwenda kwa watu wazima kote duniani ili kutoa madukuduku yao na kutanabaisha wanachokitaka kwa ajili ya mustakbali wao.Kama ulivyosikia katika taarifa yetu ya kwanza leo ni siku ya watoto duniani ikirejelea tarehe 20 Novemba mwaka 1954 kwa mara ya kwanza kabisa ilipoanzishwa na Umoja wa Mataifa kusongesha umoja na kujitambua miongoni mwa watoto duniani..Makala ikiwa leo ni siku ya watoto duniani, tunakupeleka Baku Azerbaijan katika mkutano wa 29 wa nchi wanachama wa mkataba wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi, COP29,  ambako Selina Jerobon amefuatilia mkutano wa watoto na vijana inayomulika mchango wao katika kuhakikisha mazingira bora.Mashinani katika kuadhimisha siku ya watoto duniani tunabisha hodi msitu wa Amazoni nchini Peru kwa mtoto Susan akitoa wito kwa dunia kuchukua hatua dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi kulinda msitu huo kunusuru kizazi cha watoto wa sasa na wa vizazi vijavyo katika taifa hilo.Mwenyeji wako ni Assumpta Massoi, karibu!

    10 min
  5. 1 DAY AGO

    Waraka kutoka kwa watoto: Kwenu watu wazima, kwa nini mnauruhusu mustakbali wetu kuwekwa rehani?

    Leo ni siku ya watoto duniani maudhui mwaka huu yakiwa "Kila mtoto, kila haki"na katika kuhakikisha sauti zao zinasikika kuhusu mustakbali wa utakao, shirika la Umoja wa Maataifa la kuhudumia watoto duniani UNICEF limewapa fursa ya kuandika barua kwenda kwa watu wazima kote duniani ili kutoa madukuduku yao na kutanabaisha wanachokitaka kwa ajili ya mustakbali wao.  Hao ni baadhi tu ya makumi ya watoto walioandika barua , hawa ni kutoka Gaza, Tanzania na Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo DRC ambao walishika kalamu na karatasi kufikisha ujumbe wao kwa watu wazima wa dunia ya sasa iliyoghubikwa na changamoto lukuki zinazoweka rehani mustakbali wao. Kwa mujibu wa ripoti mpya ya UNICEF ya “Hali ya watoto duniani mwaka 2024: Mustakabali wa Utoto katika Ulimwengu Unaobadilika,” iliyotolewa leo sanjari na maadhimisho ya siku hii kuna masuala matatu makubwa ya kimataifa yatakatoathiri maisha ya watoto ifikapo 2050 na kuendelea. Mosi ni mabadiliko katika idadi ya watu, pili janga la mabadiliko ya tabianchi na migogoro na tatu teknolojia UNICEF inasema yote haya ni changamoto na fursa ambazo watoto wanaweza kukabiliana nazo katika zama zijazo. Rafif mtoto mkimbizi wa ndani ameandika barua kutoka Palestina ambako vita imetamalaki, anasema “Ninatoka mjini Gaza na sasa nimefurushwa hadi Kusini mwa Gaza. kama watoto Ni haki yetu kuishi kwa usalama na kujenga mustakbali bora” Kutoka mashariki ya Kati hadi Afrika Mashariki kwa Steven akimulika afya “Na nianaandika kwenu kutoka Tanzania. Kwenye jamii yangu watoto wanaugua kila wakati , kwa nini? Huu ndio mustakbali wangu je unasikiliza?” Nako Congo DRC mitihani ni mingi, Andrea anasema “Nataka kushuhudia dunia ambayo kila mtoto anapendwa, dunia ambayo amani inashamiri ni raha na faraja. Napenda kuona hasira zinageuka na kuwa mazungumzo” Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akiunga mkono suti hizo za watoto katika ujumbe wake amesema Katika Siku ya Watoto Duniani tunasherehekea washiriki wachanga zaidi wa familia yetu ya kibinadamu. Lakini leo pia ni wakati wa kutambua changamoto kubwa zinazowakabili watoto katika ulimwengu wetu uliogawanyika sana, wenye misukosuko na mara nyingi ulioshamiri ukatili.” Ripoti ya UNICEF imetoa wito wa kuwekeza katika elimu, miji endelevu na yenye mnepo kwa watoto, miundombinu inayohimili mabadiliko ya tabianchi, teknolojia, huduma muhimu na mifumo ya msaada wa kijamii na pia teknolojia iliyo salama kwa watoto ili kupambana na mzigo wa changamoto zinazowakabili.

    2 min
  6. 2 DAYS AGO

    19 NOVEMBA 2024

    Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina inayotupeleka Baku nchini Azerbaijan kwenye mkutano wa COP29. Miongoni mwa mambo yanayopigiwa chepuo ni madini ya kimkakati yanayoelezwa kuwa ni jawabu la nishati chafuzi kwa mazingira na tunapata ufafanuzi kutoka kwa Adam Anthony, Mkurugenzi Mtendaji wa HakiRasilimali nchini Tanzania. Katibu  Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amewasihi viongozi wa kundi la nchi 20 zenye uchumi mkubwa zaidi duniani, G20 wanaokutana huko Rio De Janeiro, Brazil kuwaagiza mawaziri na washawishi wao huko COP29 wahakikishe wanakubaliana juu ya lengo jipya na kubwa la mwaka huu la ufadhili kwa tabianchi nchi. Guterres amesema sambamba na hilo ni vema kukabiliana na taarifa potofu kuhusu tabianchi.Huko Kusini mwa Lebanon, walinda amani wanaohudumu kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kikosi cha Mpito nchini humo, UNIFIL, wameshuhudia uharibifu mkubwa wa kutisha kwenye vijiji vilivyoko sambamba na eneo      la kati ya Israeli na Lebanon lisilopaswa kuwa na mapigano, huku hali ya watoto nchini humo ikizidi kuwa mbaya.Hii leo ni siku ya choo duniani ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema licha ya choo kuwa ni msingi wa kusongesha afya ya binadamu na kusaidia watoto wa k**e na wanawake kuishi maisha ya utu, bado wakazi wengi wa dunia hususan kwenye mizozo na majanga wanaishi bila huduma hiyo ya msingi.Mashinani tunasalia huko huko Baku, kwenye COP29 ambapo nampisha msichana mwanaharakati wa mazingira kutoka Tanzania, akieleza ni nini anafanya na nini atakachoondoka nacho kwenye mkutano huo.Mwenyeji wako ni Flora Nducha, karibu!

    11 min

About

Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

More From United Nations

To listen to explicit episodes, sign in.

Stay up to date with this show

Sign in or sign up to follow shows, save episodes and get the latest updates.

Select a country or region

Africa, Middle East, and India

Asia Pacific

Europe

Latin America and the Caribbean

The United States and Canada