COP29 Georgina Magesa: Watoto wana haki ya kuishi katika mazingira salama
Mkutano wa 29 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP29 unaoendelea huko Baku Azerbaijan umeleta pia watoto na vijana wanaharakati wa mazingiria kutoka kote ulimwenguni na kuwapatia fursa kuketi katika meza moja na viongozi ili kuhakikisha mustakabali wao umewekwa katika ajenda ya mkataba huo. Jukumu lao kama wachechemuzi wa mabadiliko chanya na hitaji la mazungumzo na ushirikiano kati ya vizazi lilitambuliwa rasmi katika matokeo ya Mkutano wa Zama Zijazo, SOTF mnamo Septemba 2024.Georgina Magesa, msichana mwenye umri wa miaka tisa na mwanaharakati wa mazingira, ambaye amewakilisha watoto wenzake kutoka Tanzania katika Mkutano wa 29 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP29 huko Baku, Azerbaijan. Anatoa ujumbe mahsusi akianza kwa kusistiza kuwa watoto pia wana mchango katika kutatua changamoto za mabadiliko ya tabianchi.“Watoto wenzangu duniani kote, nyie pia mnaweza kuleta mabadiliko chanya. Anza na hatua ndogo pia muwe na ndoto kubwa. Panda miti. Hifadhi maji. Jifunze kuhusu mazingira yetu. Kwa Pamoja vitendo vyetu vidogo vitageuka mabadiliko makubwa”Katika mwaka huu wa 2024 ambao viwango vya joto duniani vimevunja rekodi duniani, watoto na vijana wanaendelea kupaza sauti zao wakihimiza viongozi wa dunia kuchukua hatua za haraka zinazohitajika ili kushughulikia janga la mabadiliko ya tabianchi. Georgina anasema Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF liko mstari wa mbele, lakini sasa ni wakati wa mshikamano kwa ajili ya mazingira bora kwa watoto wa leo, na wa zama zijazo..“Kwa viongozi wa dunia walioko hapa leo, hii si kazi ya UNICEF pekee. UNICEF inafanya kazi nzuri na sisi watoto, lakini tunahitaji msaada wako ili kujenga ulimwengu wa kesho ambapo hakuna mtoto anayepaswa kuchagua kati ya afya na elimu yake; ambapo hakuna mtoto anayekunywa maji yasiyo salama; hakuna mtoto anayekosa shule kwa sababu ya masuala yanayohusiana na mabadiliko ya tabianchi; na ambapo kila mtoto ana nafasi ya kuwa na afya bora na elimu bora.”Georgina anatamatisha kwa kusisitiza kuwa janga la mabadiliko ya tabianchi limenyima watoto haki zao hivyo kwa kila mtu...“Kumbuka unapolinda mazingira unalinda afya, elimu na ndoto za watoto. Mtoto mwenye afya bora na elimu bora anaweza kubadilisha ulimwengu.”Ama kweli watoto wana haki ya kuishi katika mazingira salama!
정보
- 프로그램
- 채널
- 주기매일 업데이트
- 발행일2024년 11월 20일 오후 7:17 UTC
- 길이4분
- 등급전체 연령 사용가