Habari za UN - Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

  1. 21 hr ago

    15 JUNI 2026

    Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina inayotupeleka nchini Kenya kufuatilia ziara ya kihistoria ya Rais wa Baraza Kuu la UN, Annalena Baerbock, kwenye kituo cha kukusanya, kuchakata  na kurejeleza taka cha Korogocho (Korogocho Material Recovery Facility - MRF) kujionea namna vijana wanavyogeuza taka kuwa fursa ya kiuchumi na silaha ya kutokomeza umasikini na uhalifu mitaani.Kufuatia makubaliano ya sitisho la mapigano la kudumu baina ya Marekani na Iran yaliyotangazwa jana jumapili Juni 14, viongozi wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa wampongeza kufikiwa kwa makubaliano hayo huku wakihimiza yaheshimiwe na pia kufunguliwe upenyo maalum wa kupitisha misaada ya kibinadamu katika mlango bahari wa Hormuz huko nchini Iran.Kutoka Mashariki ya Kati twende Afrika, ambako mapigano nchini Sudan yanaelezwa kutoonesha dalili yoyote ya kupungua, huku pande zinazohasimiana zikituhumiwa kutumia mbinu za kukamatwa kiholela, mateso na kutoweshwa kwa raia kwa nguvu. Taarifa iliyotolewa leo na Tume Huru ya Umoja wa Mataifa ya Kuchunguza Ukweli kuhusu Sudan imesema vitendo hivyo vinaweza kuhesabiwa kuwa uhalifu dhidi ya ubinadamu.Na leo ni Siku ya siku ya Uelimishaji Kuhusu Ukatili dhidi ya Wazee Duniani ambapo Umoja wa Mataifa umesema hatua zaidi zinahitajika kuwalinda wazee dhidi ya ukatili, huku ukionya kuwa uelimishaji pekee hautoshi na kwamba dunia inapaswa kuimarisha sheria, huduma za afya na mifumo ya kuripoti matukio ya unyanyasaji.Mwenyeji wako ni Anold Kayanda, karibu!

    10 min
  2. 4 days ago

    11 JUNI 2026

    Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina. Mkutano wa 19 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu CRPD, umetamatishwa leo katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani. Idhaa hii imepata fursa ya kuzungumza na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya mkutano huu muhimu, Mtanzania Zuleikha Tambwe. Pia tunakuletea jifunze Kiswahili na muhtasari wa habari kama zifuatazo..Hatari ya Ebola wakati wa Kombe la Dunia la Soka 2026 ni ndogo na hakuna sababu ya mashabiki kubadili mipango yao ya safari kuelekea Canada, Mexico na Marekani, limesema Shirika la Afya Duniani WHO kombe hilo liking’oa nanga leo. Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Ulaya, Hans Henri P. Kluge, amesema hakuna wagonjwa wa Ebola katika nchi hizo wala Ulaya na amesisitiza, “Safirini kama kawaida na furahieni mashindano hayo.” WHO imefafanua kuwa Ebola haisambai kwa njia ya hewa na visa vingi vipo katika maeneo ya mbali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Annalena Baerbock, amehitimisha ziara  ya siku mbili jijini Nairobi nchini Kenya, ambapo amesisitiza nafasi muhimu ya Umoja wa Mataifa katika kuendeleza maendeleo, amani na ushirikiano barani Afrika. "Kila siku Umoja wa Mataifa na washirika wake huokoa maisha. Bila UN, mamilioni ya watoto wasingepata elimu kupitia UNICEF wala chanjo muhimu kupitia WHOna tusingekuwa na ushirikiano kama huu."Mkutano wa 19 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu CRPD, uliokuwa unafanyika hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani umefikia tamati leo. Kaulimbiu ya mwaka huu ni “kuadhimisha miaka 20 ya mkataba huo na kuimarisha utekelezaji wake katika dunia inayobadilika.” Kibaya Laibuta, Jaji wa Mahakama ya Rufani nchini Kenya, ambaye pia ni mlemavu aliyeoona au  kipofu, ameshiriki na anaeleza alivyouona mkutano huu.Katika kujifunza lugha ya Kiswahili, leo mchambuzi wetu ni Dkt. Josephat Gitonga, ambaye ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi nchini Kenya kwenye kitivo cha Tafsiri na Ukalimani anafafanua maana ya methali “Lililo lujani ni la lusu”.Mwenyeji wako ni Rashid Malekela, karibu!

    11 min
  3. 6 days ago

    09 JUNI 2026

    Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina. Kesho kutwa Alhamisi ya Juni 11, macho na masikio yanaelekezwa Mexico, Canada na hapa Marekani kwa ajili ya fainali za kombe la dunia kwa mpira wa miguu, au soka al maarufu kabumbu. Ingawa hivyo zama za sasa za mchezo huo maarufu zaidi duniani zinakumbwa na madhara ya  athari za mabadiliko ya tabianchi. Ongezeko la joto kali linavuruga mechi na kuzua wasiwasi kuhusu mustakabali wa mchezo huo. Ni kwa kuzingatia hilo, Sekretarieti ya Mkataba wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, UNFCCC inamulika suala hilo na kutoa mapendekezo ya nini kifanyike kwani hivi sasa madhara ya joto kali kwenye kabumbu ni dhahiri. Feissal Kirwa anamulika hilo kupitia video iliyoandaliwa na UNFCCC.Pia tunakuletea muhtasari wa habari na jifunze Kiswahili.Takriban watoto milioni 138 duniani kote bado wako katika ajira za watoto, wakiwemo watoto milioni 54 wanaofanya kazi hatarishi. Hayo yamo katika ripoti mpya iliyotolewa leo na Shirika la Kazi la Umoja wa Mataifa ILO. Katika ujumbe wakwe kwenye ripoti hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa ILO, Gilbert F. Houngbo, ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka ili kubadili hali hii.“Habari njema ni kwamba hadi sasa tuna wagonjwa 19 ambao wamepona, hivyo utambuzi wa mapema na matibabu vinaokoa maisha,”  Huyo ni Mkurugenzi wa Operesheni za Tahadhari na Hatua za Dharura za Afya wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani (WHO), Dkt. Abdirahman Mahamud, akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva leo kwa njia ya video kutoka Bunia katika Jimbo la Ituri, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, jimbo ambalo linachangia asilimia 94 ya wagonjwa wote wa Ebola.Mkutano wa 19 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu CRPD, umeanza leo Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York na utaendelea hadi 11 Juni. Kaulimbiu ya mwaka huu ni “kuadhimisha miaka 20 ya mkataba huo na kuimarisha utekelezaji wake katika dunia inayobadilika.” Washiriki wanajadili namna ya kutokomeza ukandamizaji, ukatili na manyanyaso dhidi ya watu wenye ulemavu, kuimarisha mifumo ya huduma na msaada, pamoja na kuongeza ushiriki na uwakilishi wao katika maisha ya kisiasa na umma.Katika kujifunza lugha ya Kiswahili hii leo Dkt Mwanahija Ali Juma, Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili, Zanzibar nchini Tanzania, BAKIZA anafafanua maana na matumizi ya neno "MKWARUZO."Mwenyeji wako ni Anold Kayanda, karibu!

    10 min

About

Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

More From United Nations