Neno la Leo

Neno la Leo 255

Hii ndiyo siku aliyoifanya Bwana (Zaburi 118:24). Anza siku mpya ya Yesu kwa kusiliza na kutafakari nasi “Neno la Leo” kila siku kwa lugha ya Kiswahili.

  1. 56m ago

    Usifikiri Mungu Amekuacha Kwa Sababu Tatizo Bado Lipo

    🎙️ Leo kwenye Neno la Leo Leo kupitia 1 Samweli 23:14 tunamkuta Daudi bado anakimbia. Sauli hajakata tamaa. Maandiko yanasema alikuwa akimtafuta Daudi kila siku. Lakini katikati ya simulizi hiyo kuna maneno machache yenye ujumbe mkubwa sana: “Lakini Mungu hakumtia mikononi mwake.” Angalia jambo hilo. Mungu hakumwondoa Sauli mara moja. Hakumaliza tatizo lote siku hiyo. Daudi bado alikuwa jangwani. Bado alikuwa anahama kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Bado kulikuwa na hatari na uncertainty. Lakini Mungu alikuwa anamshikilia katikati ya hayo yote. Mara nyingi tunafikiri ulinzi wa Mungu lazima uonekane kwa tatizo kuondoka. Tunaomba, “Bwana, niondolee hili.” Na wakati mwingine Mungu huliondoa. Lakini kuna nyakati tatizo haliondoki mara moja na Mungu anatufundisha kuona kwamba uwepo wa tatizo si ushahidi wa kutokuwepo kwake. Huenda bado hujapata jibu ulilokuwa unasubiri. Huenda bado unapambana na jambo lilelile. Huenda mazingira yako hayajabadilika kwa namna uliyotarajia. Lakini ukiangalia safari yako vizuri, huenda ukaona jambo jingine: tatizo halikuondoka mara moja lakini Mungu hakukuacha. Daudi alikuwa amepakwa mafuta kuwa mfalme lakini bado alikuwa jangwani. Sauli alikuwa na jeshi na alikuwa akimtafuta kila siku. Lakini Sauli hakuweza kumaliza kile ambacho Mungu alikuwa bado anakijenga ndani ya Daudi. Na huenda huo ndio ushuhuda wako pia. Wakati mwingine ushuhuda si, “Mungu aliondoa tatizo mara moja.” Wakati mwingine ushuhuda ni: “Nilipitia jambo ambalo nilifikiri lingenimaliza, lakini Mungu akanishikilia mpaka nikapita.” Kwa hiyo usihitimishe kwamba Mungu hayupo kwa sababu tu Sauli bado anakutafuta. Tatizo linaweza kuwa bado lipo. Lakini Mungu bado yupo. Na wakati mwingine muujiza si kwamba tatizo liliondoka. Muujiza ni kwamba tatizo halikuweza kukuondoa wewe. Karibu tusikilize, tutafakari na kujifunza pamoja. 🙏📖✨

    Usifikiri Mungu Amekuacha Kwa Sababu Tatizo Bado Lipo
  2. 1d ago

    Muulize Mungu Kabla ya Kuchukua Hatua!

    🎙️ Leo kwenye Neno la Leo Leo kupitia 1 Samweli 23:2 tunamwona Daudi akikabiliwa na uamuzi mwingine muhimu. Anaambiwa kwamba Wafilisti wanashambulia Keila na kuiba mazao yao. Daudi alikuwa na sababu nyingi za kujiamini. Huyu ndiye aliyemshinda Goliathi. Ana uzoefu wa vita. Sasa ana watu wanaomfuata. Angeweza kusikia taarifa hiyo na kusema, “Hili nalijua. Twendeni kupigana.” Lakini jambo la kwanza Daudi anafanya linatufundisha kitu muhimu sana: “Daudi akauliza kwa Bwana.” Daudi alikuwa na uwezo lakini hakuruhusu uwezo wake uchukue nafasi ya mwongozo wa Mungu. Na hapo ndipo Neno la leo linapotufikia. Kadiri tunavyopata uzoefu katika maisha, ndivyo ilivyo rahisi kuanza kutegemea kile tunachojua. “Nimeshawahi kufanya hii kazi. Najua biashara hii. Najua watu hawa. Najua mfumo. Najua namna ya kushughulikia jambo hili.” Lakini uzoefu hauondoi hitaji la kumwuliza Mungu. Kuna tofauti kati ya kusema, “Bwana, nimeamua kufanya hivi, sasa nibariki,” na kusema, “Bwana, kabla sijaamua, niongoze.” Na kumwuliza Mungu hakumaanishi kila mara tutasikia sauti kutoka mbinguni ikituambia tufanye nini. Tunatafuta mwongozo wake kupitia Neno lake, maombi, hekima, ushauri mzuri na moyo ulio tayari kutii hata jibu lake lisipokuwa lile tulilotaka. Huenda una uamuzi mbele yako kuhusu kazi, biashara, familia, mahusiano, fedha au hatua inayofuata ya maisha yako. Kabla hujakimbilia kile kinachoonekana sahihi kwa sababu tu unaweza kukifanya, simama kidogo. Umeshamuuliza Mungu? Kwa sababu si kila kitu unachoweza kufanya ndicho unachopaswa kufanya. Daudi alikuwa anajua kupigana. Lakini kabla hajapigana, alitaka kujua kama Mungu alikuwa anamtaka aende. Kwa hiyo usimtafute Mungu baada ya kufanya uamuzi ili akubariki tu. Mtafute kabla ya uamuzi ili akuongoze. Karibu tusikilize, tutafakari na kujifunza pamoja. 🙏📖✨

    Muulize Mungu Kabla ya Kuchukua Hatua!
  3. 2d ago

    Usihitimishe Hadithi Yako Ukiwa Pangoni!

    🎙️ Leo kwenye Neno la Leo Leo kupitia 1 Samweli 22:1–2 tunamkuta Daudi mahali ambapo huenda hakuwahi kufikiria angefika: katika pango la Adulamu. Fikiria safari yake. Alipakwa mafuta kuwa mfalme. Akamshinda Goliathi. Wanawake wakaimba jina lake. Akaingia katika nyumba ya mfalme na kila kitu kikaonekana kinaelekea juu. Lakini sasa yuko pangoni. Kwa macho ya kawaida, unaweza kuangalia maisha ya Daudi na kusema, “Kuna kitu kimeharibika.” Aliyeahidiwa ufalme anawezaje kuwa mkimbizi pangoni? Lakini Mungu bado hajamaliza. Akiwa katika pango hilo, watu wanaanza kuja kwa Daudi. Wenye dhiki, wenye madeni na wenye uchungu wa moyo wanakusanyika karibu naye. Takribani watu mia nne. Na Biblia inatuambia kwamba Daudi akawa kiongozi wao. Hapo ndipo tunagundua kwamba pango halikuwa tu mahali pa kujificha. Lilikuwa pia darasa la uongozi. Daudi hajapewa jeshi lililokamilika. Amepewa watu halisi wenye matatizo, majeraha na mahitaji tofauti. Na kabla hajajifunza kuongoza taifa, Mungu anamruhusu ajifunze kuongoza watu mia nne pangoni. Kabla ya kiti cha enzi, kulikuwa na pango. Na huenda hiyo ndiyo hali yako leo. Kuna mahali ulifikiri ungefika lakini maisha yako hayaonekani kuelekea huko. Kuna jambo ulilokuwa na uhakika Mungu analifanya lakini mazingira ya sasa yanaonekana kinyume kabisa. Usihitimishe hadithi yako ukiwa pangoni. Kwa sababu wakati mwingine mahali tunapofikiri tumefichwa ndipo Mungu anapotujenga. Kipindi unachotaka kimalizike haraka kinaweza kuwa kinakuza ndani yako tabia, hekima, uvumilivu na uwezo utakaohitaji katika hatua inayofuata. Daudi bado hajafika kwenye kiti cha enzi. Lakini pangoni tayari anaanza kujifunza kuwa mfalme. Kwa hiyo usidharau pango lako. Usifikiri Mungu amekuacha kwa sababu mazingira ya sasa hayafanani na ahadi. Huenda bado hujaona kile Mungu anachokupeleka kuwa, lakini tayari anatumia mahali ulipo kukutengeneza kwa ajili yake. Karibu tusikilize, tutafakari na kujifunza pamoja. 🙏📖✨

    Usihitimishe Hadithi Yako Ukiwa Pangoni!
  4. 3d ago

    Hata Watu wa Imani Huogopa!

    🎙️ Leo kwenye Neno la Leo Leo kupitia 1 Samweli 21:12–13 tunakutana na upande tofauti kabisa wa Daudi. Huyu ndiye Daudi aliyesimama mbele ya Goliathi wakati jeshi lote la Israeli limejaa hofu. Huyu ndiye aliyesema, “Ninakujia kwa jina la Bwana.” Huyu ndiye aliyetangaza, “Vita ni vya Bwana.” Lakini leo Biblia inatuambia kwamba Daudi akaogopa sana. Akiwa anakimbia kutoka kwa Sauli, anafika Gathi na anapotambua hatari aliyomo, hofu inamjaa kiasi kwamba anajifanya mwendawazimu ili kuokoa maisha yake. Huyu bado ni Daudi. Na hilo linatufundisha jambo muhimu sana: kuwa na imani hakumaanishi kwamba hutawahi kuogopa. Kuna siku utasimama mbele ya “Goliathi” wako ukiwa na ujasiri mkubwa. Lakini kuna siku nyingine jambo fulani litakufanya moyo wako utetemeke. Kuna siku utaomba ukiwa na confidence kubwa na siku nyingine utaomba ukiwa umechoka, una maswali na hujui mambo yatakuwaje. Hilo halimaanishi kila kitu ambacho Mungu amekuwa akijenga ndani yako kimepotea. Kwa hiyo swali si tu, “Je, ninaogopa?” Swali muhimu zaidi ni, “Nitafanya nini na hofu yangu?” Usijifiche mbele za Mungu. Usijifanye una nguvu wakati ndani umechoka. Mpelekee Mungu kile kinachokutisha. Mwambie ukweli: “Bwana, hili linaniogopesha. Sijui litakuwaje lakini bado nitakutegemea.” Kwa sababu imani si kila wakati kusema, “Siogopi.” Wakati mwingine imani ni kusema: “Naogopa, lakini hofu yangu haitakuwa mwisho wa simulizi yangu. Bado nitamtafuta Mungu. Bado nitamwomba. Bado nitamtegemea.” Daudi aliyemwamini Mungu mbele ya Goliathi ndiye Daudi tunayemwona akiogopa leo. Na Mungu bado hajaacha kufanya kazi katika maisha yake. Kwa hiyo usijilaumu kwa sababu leo unaogopa jambo ambalo jana ulifikiri ungeweza kulikabili. Mpelekee Mungu hofu yako. Naogopa, lakini bado nitamtegemea Mungu. Karibu tusikilize, tutafakari na kujifunza pamoja. 🙏📖✨

    Hata Watu wa Imani Huogopa!
  5. 4d ago

    Rafiki Yako Akifanikiwa Kuliko Wewe, Bado Utamshangilia?

    🎙️ Leo kwenye Neno la Leo Leo kupitia 1 Samweli 20:17 tunaendelea kuangalia urafiki wa ajabu kati ya Daudi na Yonathani. Maandiko yanatuambia kwamba Yonathani alimpenda Daudi kama alivyoipenda nafsi yake mwenyewe na akamtaka athibitishe tena kiapo chao. Lakini kuna kitu kinachoufanya urafiki huu kuwa wa kipekee zaidi. Yonathani alikuwa mwana wa mfalme. Kwa kawaida angeweza kutarajia kwamba siku moja angechukua nafasi ya baba yake. Lakini kadiri Daudi anavyosogea katika kusudi la Mungu juu ya maisha yake, ndivyo uwezekano wa Yonathani kuwa mfalme unavyopungua. Yonathani angeweza kumwangalia Daudi na kuona competitor. Badala yake, alimwona rafiki. Na hapo ndipo urafiki unapopimwa. Ni rahisi kumshangilia rafiki yako anapoanza biashara. Lakini biashara yake ikianza kufanya vizuri kuliko yako je? Ni rahisi kumpongeza anapopata nafasi nzuri. Lakini akipata nafasi ambayo wewe pia uliitamani je? Ni rahisi kufurahia maendeleo ya mtu mpaka maendeleo yake yanapoanza kugusa eneo ambalo wewe pia ulitamani kufanikiwa. Watu wengi wanaweza kushangilia ushindi wako mpaka ushindi wako uanze kugusa nafasi yao. Lakini Yonathani anatufundisha kwamba rafiki si competitor wako kwa sababu tu Mungu anafanya jambo kubwa katika maisha yake. Baraka yake haimaanishi kushindwa kwako. Dunia inatufundisha kuuliza, “Mtu huyu anaweza kunisaidiaje?” Urafiki wa kweli unauliza, “Ninawezaje kuwa mwaminifu kwake hata kama hakuna faida ninayopata?” Na huenda leo tunahitaji kujiuliza swali gumu kidogo: Rafiki yangu akifanikiwa kuliko mimi, bado nitaweza kumshangilia kwa moyo safi? Kwa sababu upendo wa kweli hauishii pale mafanikio ya mwingine yanapoanza kutugharimu. Yonathani hakumgeuza Daudi kuwa mshindani kwa sababu tu Mungu alikuwa akimwinua. Huo ndio moyo tunaohitaji: moyo unaoweza kusema, “Kama Mungu anakufungulia mlango, nitafurahi pamoja nawe. Sitafanya baraka yako kuwa tishio kwangu.” Karibu tusikilize, tutafakari na kujifunza pamoja. 🙏📖✨

    Rafiki Yako Akifanikiwa Kuliko Wewe, Bado Utamshangilia?
  6. 5d ago

    Rafiki wa Kweli Anakutetea Hata Usipokuwepo!

    🎙️ Leo kwenye Neno la Leo Leo kupitia 1 Samweli 19:4–5 tunamwona Yonathani akifanya jambo linalotuonyesha maana nyingine ya urafiki wa kweli. Sauli sasa anataka Daudi auawe. Daudi hayupo kwenye mazungumzo haya lakini Yonathani yupo. Na badala ya kukaa kimya, anamkumbusha baba yake ukweli: Daudi hajamkosea. Anamkumbusha jinsi Daudi alivyohatarisha maisha yake kupigana na Goliathi na jinsi Mungu alivyotumia ushindi wake kuleta furaha kwa Israeli. Lakini kuna jambo kubwa zaidi hapa. Yonathani angeweza kufaidika Daudi akiondolewa. Kama mwana wa Sauli, alikuwa na maslahi yake mwenyewe katika kiti cha enzi. Hata hivyo, Yonathani anachagua kilicho sahihi kuliko kile kinachoweza kumnufaisha yeye. Huo ndio urafiki wa kweli. Ni rahisi sana kumwambia mtu, “Wewe ni rafiki yangu,” akiwa mbele yetu. Lakini kipimo kingine cha urafiki kinakuja pale jina lake linapotajwa akiwa hayupo. Watu wakianza kumsema vibaya, tunafanya nini? Tunajiunga nao? Tunakaa kimya ili tusiharibu nafasi yetu kwenye kundi? Au tunakuwa na ujasiri wa kusema, “Hapana, hicho mnachosema si sahihi”? Kutetea rafiki hakumaanishi kuficha makosa yake. Rafiki wa kweli anaweza kukuambia ukweli unapokosea. Lakini pia hataruhusu uongo usemwe juu yako wakati anajua ukweli. Na huenda leo swali si tu, “Nina rafiki kama Yonathani?” Swali kubwa zaidi linaweza kuwa: “Mimi ni Yonathani kwa nani?” Je, watu ninaowaita marafiki wanaweza kuwa na uhakika kwamba hata wakiwa hawapo, sitatumia udhaifu wao kujinufaisha, sitajiunga na wanaowasema vibaya na nitasimamia ukweli? Kwa sababu rafiki wa kweli si yule anayesema mazuri kuhusu wewe ukiwepo tu. Ni yule anayesimamia ukweli hata ukiwa haupo. Karibu tusikilize, tutafakari na kujifunza pamoja. 🙏📖✨

    Rafiki wa Kweli Anakutetea Hata Usipokuwepo!
  7. 6d ago

    Unaweza Kufanikiwa Bila Kumpoteza Mungu Njiani!

    🎙️ Leo kwenye Neno la Leo Leo kupitia 1 Samweli 18:14 tunakutana na maneno machache lakini yenye ujumbe mkubwa sana kuhusu maisha ya Daudi: “Daudi akafanikiwa katika njia zake zote, naye Bwana alikuwa pamoja naye.” Ni rahisi kusimama kwenye sehemu ya kwanza, “Daudi akafanikiwa.” Lakini siri ya maisha yake ipo katika sehemu inayofuata: “Bwana alikuwa pamoja naye.” Mwezi huu tumemfuata Daudi kutoka malishoni. Tulimwona akiwa kijana asiyepewa nafasi kubwa hata ndani ya familia yake. Akaingia ikulu. Akasimama mbele ya Goliathi. Akapata ushindi na jina lake likaanza kujulikana katika Israeli. Sasa Sauli anaanza kumwonea wivu na kumwangalia kwa mashaka. Mazingira ya Daudi yanaendelea kubadilika lakini uwepo wa Mungu unabaki kuwa msingi wake. Na hapa kuna swali muhimu kwetu. Tunapotafuta maendeleo, fedha, cheo, biashara inayokua, recognition na milango mipya, je, tunatafuta pia kuhakikisha kwamba tunabaki karibu na Mungu? Kwa sababu inawezekana kupata kile tulichokuwa tunakiomba lakini njiani tukapoteza kitu cha thamani zaidi. Ndiyo maana Yesu anauliza, “Itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote na kupata hasara ya nafsi yake?” Mafanikio ya kweli si kuwa na kila kitu huku moyo wako ukiwa mbali na Mungu. Mafanikio makubwa ni kufika unakokwenda bila kumpoteza Mungu njiani. Kwa hiyo leo usiombe tu, “Bwana, nifanikishe.” Omba pia, “Bwana, ninapopanda, ninapofanikiwa na ninapofunguliwa milango mipya, nisaidie nibaki karibu nawe.” Kwa sababu mwisho wa yote, jambo kubwa zaidi linaloweza kusemwa kuhusu maisha yetu si tu kwamba “alifanikiwa.” Ni kwamba: “Alifanikiwa, naye Bwana alikuwa pamoja naye.” Karibu tusikilize, tutafakari na kujifunza pamoja. 🙏📖✨

    Unaweza Kufanikiwa Bila Kumpoteza Mungu Njiani!
  8. Sep 14

    Usiruhusu Wivu Uharibu Moyo Wako!

    🎙️ Leo kwenye Neno la Leo Leo kupitia 1 Samweli 18:7–9 tunaona mabadiliko ya kusikitisha yakianza ndani ya moyo wa Sauli. Baada ya ushindi, wanawake wanaimba wakisema Sauli amewaua maelfu yake na Daudi makumi ya maelfu yake. Sauli anasikia comparison hiyo na kuanzia hapo anaanza kumwangalia Daudi kwa jicho tofauti. Lakini Daudi hajamkosea Sauli. Tatizo ni kwamba mafanikio ya Daudi yameanza kumfanya Sauli ajisikie mdogo. Na hapo ndipo wivu huanzia mara nyingi. Mtu mwingine anapata promotion na badala ya kufurahi tunaanza kujiuliza, “Kwa nini si mimi?” Biashara yake inakua. Anaolewa au anaoa. Anapata mtoto. Ananunua nyumba. Anapata nafasi tuliyoitamani au anatambuliwa na watu. Ghafla, kitu kizuri kinachotokea katika maisha yake kinaanza kutuumiza sisi. Lakini kumbuka hili: baraka ya mtu mwingine si ushahidi kwamba Mungu amekusahau. Safari yake si kipimo cha safari yako. Mungu kufanya jambo zuri katika maisha ya mtu mwingine hakupunguzi kile anachoweza kufanya katika maisha yako. Sauli alianza kwa kusikia wimbo. Kisha akaanza kumwangalia Daudi kwa mashaka. Na baadaye wivu huo utakua na kuathiri maamuzi yake. Hapo tunajifunza kwamba wivu usiposhughulikiwa mapema unaweza kubadilisha namna tunavyomwona mtu ambaye hajatutendea chochote. Kwa hiyo linda moyo wako mapema. Unapoona mwingine akibarikiwa, jifunze kufurahi pamoja naye. Mwambie Mungu kwa moyo wa kweli, “Asante Bwana kwa kile unachofanya katika maisha yake. Na mimi nitaendelea kuwa mwaminifu katika safari uliyonipa.” Huhitaji kuzima mwanga wa mtu mwingine ili wako uangaze. Mungu hajakusahau kwa sababu tu leo ni zamu ya mwingine kusherehekea. Karibu tusikilize, tutafakari na kujifunza pamoja. 🙏📖✨

    Usiruhusu Wivu Uharibu Moyo Wako!

About

Hii ndiyo siku aliyoifanya Bwana (Zaburi 118:24). Anza siku mpya ya Yesu kwa kusiliza na kutafakari nasi “Neno la Leo” kila siku kwa lugha ya Kiswahili.