Habari za UN - Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

  1. 2d ago

    02 OKTOBA 2026

    Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina. Mwaka huu ni miaka 75 tangu ulipopitishwa mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Wakimbizi mwaka 1951 na tangu wakati huo mamilioni ya wakimbizi wamepatiwa hifahi, usalama na maisha yao kuokolewa na kubadilishwa kupitia mpango wa mkataba huo wa kuwapeleka wakimbizi katika nchi ya tatu kuanza upya maisha yao. Miongoni mwa wafaidika wa mpango huo ni mgeni wetu kwenye mada ya leo aliyekimbia vita Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, hadi Uganda na kisha nchini Sweden ambako sasa ni mwanaharakati wa kuchagiza haki za wakimbizi, mwanamuziki na Balozi mwema wa Kitaifa wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR. Pia tunakuletea muhtasari wa habari. • Takribani watoto wakimbizi milioni 5.8, sawa na asilimia 44 ya watoto wakimbizi milioni 13.1 wenye umri wa kwenda shule duniani, hawakuwa shuleni mwaka 2025, kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa leo na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR). Ripoti inaonya kuwa kupungua kwa ufadhili wa kibinadamu na maendeleo kunaweza kuwaweka mamilioni zaidi nje ya madarasa na kurudisha nyuma mafanikio yaliyopatikana kwa miaka mingi katika elimu ya wakimbizi.. • Sakata usafirishaji bidhaa kwa njia ya meli kwenye Mlango wa Bahari wa Hormuz utasababisha wanawake na wasichana wengine milioni 11.7 katika nchi 28 duniani kukabiliwa na ukosefu wa chakula ifikapo mwishoni mwa mwaka huu. Akiwasilisha uchambuzi wa shirika hilo katika mataifa hayo yakiwemo ya Afrika, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa UN Women, Nyaradzayi Gumbonzvanda, [NYARAZAYI GUMBOVANDA] amesema vyakula vimepanda bei kutokana na ongezeko la gharama za usafirishaji,na kwamba “uzoefu wa migogoro iliyopita unaonesha kuwa chakula kinapopungua, wanawake mara nyingi hupunguza kiasi wanachokula au wanakula mwisho au wanaruka mlo ili kupatia kipaumbele watu wengine.”. • Na hii leo shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani, WHO, limetoa ripoti inayoonesha magonjwa 10 yaliyoongoza duniani mwaka 2023 kwa kusababisha vifo na 10 yanayoongoza kwa kusababisha mtu kubadili mwenendo wa maisha licha ya kubainika kuwa umri wa kuishi duniani umeongezeka. Magonjwa 10 kwa mpangilio kwa kuongoza vifo duniani ni magonjwa ya kuziba kwa mishipa ya moyo, kiharusi, ugonjwa wa mapafu, maambukizi katika njia ya hewa, ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu, kisukari, saratani ya koo na mapafu, shinikizo la damu, magonjwa ya figo na kuhara.” Mwenyeji wako ni Assumpta Massoi, karibu!

  2. 3d ago

    01 OKTOBA 2026

    Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina. Miongoni mwa mikutano iliyochukua nafasi kubwa wakati wa Mjadala Mkuu wa ngazi ya juu wa Kikao cha 81 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa , UNGA81 ni kuhusu Akili Mnembaa u AI. Pamoja na changamoto zake lakini AI inauweza mkubwa wa kusaidia jamii kutatua changamoto na hata kuondoa taarifa potofu. Waandishi wa habari hawakuachwa nyuma nao walikuwa na mikutano kadhaa kujadili namna watakavyotumia taalum yao kuisaidi jamii. Mwenzangu Leah Mushi amezungumza na Rais wa wahariri wa habari barani Afrika Churchill Otieno aliyehudhuria mikutano kuhusu ubora wa habari pamoja na akili mnemba AI kwa tasnia ya habari. Kwanza anaanza kwa kueleza kubwa lililozungumzwa kwenye mikutano hiyo? Pia tunakuletea muhtasari wa habari. • Usiku wa kuamkia jana Jumatano kituo cha kutibu Ebola kwenye kituo cha mpito cha kuhifadhi wakimbizi huko Kigonze, karibu na mji wa Bunia jimboni Ituri, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, (DRC), kilichomwa moto, wakati huu ambapo kimesalia kitupu kutokana na wakimbizi kukimbia mashambulio ya mara kwa mara kutoka makundi yaliyojihami.. • Leo ikiwa ni siku ya wazee duniani wakati huu ikielezwa kwamba kila mtu ni mzee mtarajiwa, na ujumbe wa mwaka huu ukiwa “Enzi ya Maisha Marefu: Kufikiria Upya Mifumo kwa Maisha Marefu,” Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amesema ongezeko la watu wanaoishi muda mrefu linahitaji serikali na taasisi kubadili mifumo ya kijamii na kiuchumi ili kukidhi mahitaji yao. Guterres amesema maisha marefu yatakuwa ni mafanikio makubwa kwa jamii pale tu yanapowezeshwa na maendeleo ya huduma za afya na mifumo ya ulinzi wa kijamii. • Na leo pia ni siku ya kahawa duniani, ikiwa ni maadhimisho ya kwanza tangu yapitishwe na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka huu. Lengo ni kuangazia zao hilo ambalo sio tu kiburudisho bali pia mbinu ya kujipatia kipato kwa kaya zipatato milioni 25 kwenye nchi zinazoendelea. Brazili, Viet Nam, Colombia zinaongoza kwa uzalishaji wa kahawa, ilhali Marekani na Muungano wa Ulaya zinaongoza kwa kuagiza na kunywa kahawa.” Mwenyeji wako ni Flora Nducha, karibu!

  3. 4d ago

    30 SEPTEMBA 2026

    Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina, tukimsikiliza mmoja wa washiriki wa UNGA81ulioanza tarehe 22 Septemba na kufunga pazia Jumatatu, tarehe 28 Septemba mwaka huu wa 2026 Paul Siniga, ambaye pamoja na wadhifa mwingine alionao ni mchechemuzi wa Tanzania katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu SDGs na mleta mabadiliko wa watoto kupitia shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF Tanzania. Kwanza anaanza kwa kueleza kilichomgusa zaidi katika mkutano wa mwaka ulikuwa na mambo mengi ikiwemo hotuba za viongozi wa ngazi za juu wa nchi na serikali pamoja na mikutano mbalimbali kandoni mwa hotuba hizo yote haya kuhakikisha mustabali wa dunia yenye umoja , utulivu na maendeleo. Lakini je vijana wanazungumziaje mkutano huo? Pia tunakuletea muhtasari wa habari. • Watoto nchini Lebanon wanakabiliwa na njaa mtoto 1 kati ya 5 akilala bila kula, kukosa shule na kulazimika kufanya kazi kutokana na umaskini unaochochewa na mgogoro, limeonya Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF. Shirika hilo limesema asilimia 14 ya kaya zina angalau mtoto mmoja anayelazimika kufanya kazi, zaidi ya mara mbili ya kiwango cha Januari 2025. UNICEF imeitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za haraka na za kudumu kulinda afya, elimu na ustawi wa watoto wa Lebanon. • Uzoefu wa miaka 15 unaonesha kuwa kuongeza kodi za tumbaku kunaweza kupunguza uvutaji wa sigara na kuongeza mapato ya serikali, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO). Uchambuzi katika nchi 15 kati ya 2009 na 2025 umeonesha kuwa matokeo makubwa zaidi yalipatikana pale serikali zilipoongeza kodi kwa kiwango kikubwa na mara kwa mara. Dkt. Etienne Krug wa WHO, amesema “Ushahidi uko wazi, serikali zinapofanya bidhaa hatarishi kuwa ghali zaidi, watu hutumia kidogo, maisha yanaokolewa na mapato ya umma huongezeka,” akitaka ongezeko la kodi linalotabirika ili kufanya tumbaku, pombe na vinywaji vyenye sukari kuwa ghali zaidi. • Na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO kwa kushirikiana na serikali ya Kenya wamezindua Mradi uitwao SoilFer unaohusisha kuwa na ramani ya aina za udongo za taifa hilo la Afrika Mashariki kwa lengo la kuwa na mfumo wa kilimo chenye mnepo. Akizungumzia mpango huo jijini Nairobi, Kenya Naibu Mkurugenzi wa FAO anayeongoza kitengo cha Ardhi na Maji Nora Berrahmouni, amesema taarifa kutoka mpango huo zinasaidia wakulima “kufahamu, mazao watakayopanda, mahali pa kupanda, jinsi ya kupanda, kiasi cha mbolea kinachohitajika na aina ya mbolea.” Mwenyeji wako ni Anold Kayanda, karibu!

  4. 5d ago

    29 SEPTEMBA 2026

    Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina. Dunia hivi sasa imegubikwa na mazingira ya uhalifu yanayozidi kuwa magum ukila uchao. Umoja wa Mataifa unasema kutokana na mazingira hayo huduma, miundombinu na teknolojia vinaweza kutumiwa vibaya na wahalifu. Hii ni pamoja na mienendo mipya inayojulikana kama “uhalifu kama huduma” na “vurugu kama huduma. Ni kwa kuzingatia hilo, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuzuia dawa za kulevya na uhalifu, (UNODC) imeitisha mkutano wa 15 huko Abu Dhabi kusaka mbinu za kisasa za kuweza kukabili uhalifu unaotumia mbinu za kisasa. Ili kubaini mengine mengi ya mkutano huo Ezzat El Feri wa Idhaa ya Kiarabu ya Umoja wa Mataifa alizungumza na Mkuu wa UNODC na mahojiano hayo ndio msingi wa mada kwa kina hii inayoletwa kwako na Assumpta Massoi? Pia tunakuletea muhtasari wa habari. • Asubuhi hii ya saa za New York-Marekani hapa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa unafanyika mkutano kuhusu Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Kabisa Silaha za Nyuklia. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ametoa wito kwa ulimwengu akisema, tunapoadhimisha siku hii muhimu, ni wakati wa kuweka njia mpya. Nchi zinazomiliki silaha za nyuklia lazima zirudi kwenye mazungumzo ili kuzuia matumizi yoyote ya silaha za nyuklia. • Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya kuelimisha umma kuhusu madhara ya upotevu na utupaji wa chakula, shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira, UNEP linasema teknolojia ya akili mnemba, (AI) imeanza kutumika kusaidia kuondokana na tatizo hilo wakati huu ambapo takwimu zinaonesha kwamba asilimia 13 ya chakula hupotea baada ya kuvunwa na kabla ya kufika madukani ilhali asilimia nyingine 19 ikipotezwa majumbani, kwenye maduka makubwa na migahawa. Michael Muratha ambaye ni Meneja Mradi kutoka UNEP kitengo cha Mabadiliko ya Tabianchi anafafanua matumizi hayo ya akili mnemba. • Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) limesema idadi ya maambukizi ya Ebola ya virusi vya Bundibugyo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, (DRC) bado iko juu licha ya dalili za kupungua kwa uenezaji wa ugonjwa huo katika baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa na mlipuko. Akizungumza mjini Geneva, Uswisi leo hii leo, Dkt. Janet Diaz, Mkuu wa Kitengo cha Huduma katika Mpango wa Dharura za Afya wa WHO, amesema, “tunajua kwamba kwa ugonjwa wa Ebola, kupata huduma za matibabu mapema kunaweza kuongeza kwa kiasi kikubwa uwezekano wa kupona. Hata hivyo, katika mlipuko huu, watu wengi bado wanafariki dunia wakiwa majumbani au katika jamii zao kwa sababu hawawezi kufika kwenye vituo vya afya kwa wakati.”. Mwenyeji wako ni Flora Nducha, karibu!

  5. 6d ago

    28 SEPTEMNA 2026

    Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina. Hii leo tunaangazia sekta ya afya barani Afrika na kuzungumzia hilo mwenzangu Leah Mushi amezungumza na Mkurugenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni Kanda ya Afrika Profesa Mohamed Janabi. Suala la kwanza kutaka kufangamu kutoka kwake ni je mkutano wa Ngazi ya Juu kuhusu maandalizi dhidi ya majanga ya milipuko ya magonjwa ulifanyika mwishoni mwa wiki hii umefikia azimio walilotaka kukubaliana? Pia tunakuletea muhtasari wa habari. • Hii leo viongozi wa nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa wanashiki kwenye Mkutano wa Ngazi ya Juu ukimulika maadhimisho ya miaka 25 na Mpango wa Utekelezaji wa Azimio la Durban la mwaka 2001 ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema anasikitishwa kuona kwamba ubaguzi wa rangi bado unaendelea duniani, na kwamba kitendo hicho kinahatarisha juhudi za kujenga dunia yenye amani, usawa na heshima kwa watu wote. Akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano huo leo kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa kando ya Mjadala Mkuu, (UNGA81) Guterres amesema ubaguzi wa rangi bado “unatia sumu” katika jamii, unazidisha pengo la kijamii na kiuchumi, na kuwanyima watu haki na uhuru wao wa msingi. • Leo ni siku ya mwisho ya Mjadala Mkuu wa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, (UNGA81). Miongoni mwa nchi zilizohutubia asubuhi hii ya saa za New York-Marekani ni Mali ambayo imewakilishwa na Waziri wake wa mambo ya nje Abdoulaye Diop ambaye pamoja na mambo mengine ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kutokaa kimya mataifa mengine yanapoingilia uhuru w anchi za Afrika akitoa mfano wa Ukraine kuunga mkono makundi ya kigaidi dhidi ya Mali. Amesisitiza hakupaswi kuwa na kitu cha “ugaidi mzuri na ugaidi mbaya.”. • Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Eritrea, Osman Saleh Mohammed, akihutubia mjadala huo mkuu amezungumza masuala mengi ambayo Umoja wa Mataifa unapaswa kuyashughulikia akitoa mfano wa athari za kile alichokiita sera ya “MAGA” ya Rais wa Marekani Donald Trump ni miongoni mwa matukio yanayohitaji kuangaliwa katika hali ya sasa ya kimataifa. Aidha ametoa wito wa kusitishwa kwa vita vinavyoendelea katika kanda mbali ukiwemo ukanda wa Sahel, Pembe ya Afrika, Mashariki ya Kati na Ukraine. Mwenyeji wako ni Flora Nducha, karibu!

  6. Sep 25

    25 SEPTEMBA 2026

    Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina. Hapa katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa leo unafanyika mkutano wa Ngazi ya Juu kuhusu maandalizi dhidi ya majanga ya milipuko ya magonjwa na kama nilivyokudokeza kuwa tutakuwa na maoni na ushauri wa baadhi ya wananchi wa Afrika Mashariki kwa viongozi wanaoshiriki mkutano huo, tunaanzia nchini Uganda, kisha tuelekee nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC. Pia tunakuletea muhtasari wa habari. • Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo linafanya Mkutano wa Ngazi ya Juu kuhusu Kuzuia, Kujiandaa na Kukabiliana na Magonjwa ya Milipuko, unaolenga kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kupitisha tamko la kisiasa kuhusu maandalizi na mwitikio wa magonjwa ya milipuko. Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Antonio Guterres, Naibu Katibu Mkuu Amina J. Mohammed amesema dunia inahitaji mshikamano, usawa na hatua madhubuti za kimataifa ili kutomwacha mtu yeyote nyuma na kujifunza kutokana na uzoefu wa hivi karibuni akisema “Janga la COVID-19 lilitufundisha kwamba, katika dunia yetu iliyounganishwa, hakuna nchi inayoweza kujilinda yenyewe. Tulijifunza jambo hili kwa gharama kubwa sana ya kibinadamu na kiuchumi.” • Tukielekea Afrika, Hama hama ya watu kutokana na mapigano mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, inmelilazimu Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, IOM, kuongeza ufuatiliaji wa Ebola katika mipaka, vituo vya wakimbizi na njia za usafiri. Hadi Septemba 21, zaidi ya watu 7,700 walikuwa wamethibitishwa kuwa na Ebola, huku 3,700 wakifariki. • Na nchini Yemen takriban watoto milioni 2.2 wenye umri wa chini ya miaka 5 wanakumbwa na utapiamlo kila uchao hawajui pa kula wala pa kulala kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF likisistiza kuwa usalama ndio kipaumbele ili watoto hao waweze kuishi kama Watoto. Akizungumza Geneva Uswisi kwa njia ya video kutoka Aden, Yemen Mwakilishi wa UNICEF nchini humo, Akhil Iyer, amesema “Tunashuhudia ongezeko la utapiamlo mkali mtoto 1 kati ya 4 anautapiamlo mkali na Watoto 200 wako katika hali mbaya sana ya unyafuzi.” Mwenyeji wako ni Leah Mushi, karibu!

Ratings & Reviews

5
out of 5
5 Ratings

About

Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

More From United Nations