Neno la Leo

Neno la Leo 255

Hii ndiyo siku aliyoifanya Bwana (Zaburi 118:24). Anza siku mpya ya Yesu kwa kusiliza na kutafakari nasi “Neno la Leo” kila siku kwa lugha ya Kiswahili.

  1. 3h ago

    Mungu Haangalii Sura, Anaangalia Moyo Wako!

    🎙️ Leo kwenye Neno la Leo Leo kupitia 1 Samweli 16:7 tunaanza mwezi mpya na hatua mpya katika simulizi ya 1 Samweli. Agosti tuliimaliza na Sauli, mtu aliyeanza vizuri lakini ambaye hatua kwa hatua alianza kuweka maamuzi yake mbele ya utiifu kwa Mungu. Sasa Samweli ametumwa nyumbani kwa Yese kumtafuta mfalme mwingine. Anapomwona Eliabu, Samweli anavutiwa na kile kinachoonekana kwa macho. Anaonekana kama mtu anayefaa kuwa mfalme. Lakini Mungu anamfundisha jambo ambalo litakuwa msingi wa safari yetu na Daudi: mwanadamu huangalia sura ya nje lakini Bwana huangalia moyo. Na hapo ndipo tunapoanzia Septemba: moyoni. Tunaishi katika dunia inayotufundisha kujenga kile watu wanaweza kuona. Muonekano, elimu, cheo, fedha, mafanikio, followers na namna tunavyoonekana mbele za wengine. Lakini Mungu anaona mahali ambapo hakuna mwanadamu anayeweza kuona kikamilifu. Anaona nia zetu, tamaa zetu, sababu zinazotusukuma kufanya tunayofanya na tabia yetu wakati hakuna anayetuangalia. Hii ndiyo tofauti tutakayoanza kuiona kati ya Sauli na Daudi. Siyo kwamba Daudi alikuwa mkamilifu. Tutakuja kuona makosa yake pia. Lakini Mungu alikuwa akitafuta moyo unaoweza kumrudia, kumsikiliza na kutengenezwa naye. Kwa hiyo tunapoanza mwezi huu, labda kabla hatujamwomba Mungu abadilishe kazi yetu, biashara yetu, mahusiano yetu au mazingira yetu, tuanze na ombi la ndani zaidi: “Bwana, tengeneza moyo wangu.” Na swali letu la kwanza la Septemba liwe hili: Mungu akiangalia moyo wangu leo, anaona nini? Kwa sababu watu wanaweza kuvutiwa na kile kilicho nje lakini Mungu huanzia ndani. Karibu tusikilize, tutafakari na kujifunza pamoja. 🙏📖✨

    Mungu Haangalii Sura, Anaangalia Moyo Wako!
  2. 1d ago

    Kuanza Vizuri Haitoshi, Linda Imani Yako Mpaka Mwisho!

    🎙️ Leo kwenye Neno la Leo Leo kupitia 1 Samweli 15:35 tunafunga safari yetu ya mwezi wa Agosti katika sehemu yenye huzuni. Samweli anamwombolezea Sauli na tunaona huzuni iliyotokana na mwelekeo ambao maisha ya Sauli yalikuwa yamechukua. Ni mwisho mzito lakini wenye somo muhimu sana: si muhimu tu kuanza vizuri, ni muhimu kuendelea kutembea na Mungu. Tulianza mwezi huu na Hana, mwanamke aliyefika mbele za Mungu akiwa na maumivu, akamimina moyo wake kwake na kujifunza kusubiri. Tukaona Mungu akimjibu na kupitia Samweli tukajifunza kusikiliza sauti ya Mungu, kumtii, kukumbuka Ebenezeri zetu na kuendelea kuwa waaminifu. Kisha tukamwona Sauli. Alianza akiwa mtu aliyepewa nafasi kubwa na Mungu. Lakini hatua kwa hatua presha, hofu ya watu na utiifu wa masharti vikaanza kuathiri safari yake. Na tunapofika mwisho wa sura ya 15, tunakutana na matokeo ya mwelekeo huo. Hili linaweza kuwa somo kubwa tunalobeba tunapofunga Agosti: ushindi wa jana hauondoi hitaji la utiifu wa leo. Hatutosheki kusema tulianza vizuri, tuliwahi kuwa karibu na Mungu au Mungu aliwahi kututumia. Kila siku tunahitaji kuendelea kumruhusu Mungu atengeneze mioyo yetu. Paulo alipofika mwisho wa safari yake alisema, “Mwendo nimeumaliza, imani nimeilinda.” Hilo liwe ombi letu pia. Si kwamba hatutakosea njiani bali tunapoanguka tunamrudia Mungu na kuendelea kutembea naye. Tunapofunga mwezi huu, swali letu liwe: Si tu nilianzaje, bali ninaendeleaje? Je, moyo wangu bado unamsikiliza Mungu? Je, bado niko tayari kumtii? Tusiombe tu Mungu atusaidie kuanza vizuri. Tumwombe atupe neema ya kubaki waaminifu na kumaliza vizuri. Karibu tusikilize, tutafakari na kujifunza pamoja. 🙏📖✨

    Kuanza Vizuri Haitoshi, Linda Imani Yako Mpaka Mwisho!

About

Hii ndiyo siku aliyoifanya Bwana (Zaburi 118:24). Anza siku mpya ya Yesu kwa kusiliza na kutafakari nasi “Neno la Leo” kila siku kwa lugha ya Kiswahili.