Ni Salama

Adrian Nzamba

Ni salama rohoni mwangu ni Podcast inayokusaidia kuboresha mahusiano yako na Mungu kupitia mafundisho mbalimbali yanayotolewa na wahubiri, walimu na wachungaji kiganjani mwako. Tunakusaidia kuweza kuanza siku vyema ukiwa na neno la mungu kama taa itakayokuwa ikikuongoza katika shughuli zako za kila siku. Kupitia Ni Salama tutakuletea mafunzo na masomo yatakayokuwezesha kuelewa zaidi neno la Mungu linalopatikana kwenye Biblia huku tukikuongezea hamu na mvuto wa kuisoma Biblia yako. Karibu

  1. EPISODE 1

    Akili kufungwa na shetani ili usifikie malengo yako

    AKILI KUFUNGWA NA SHETANI. Luka 8:26‭-‬39 “Wakafika pwani ya nchi ya Wagerasi, inayoelekea Galilaya. Naye aliposhuka pwani, alikutana na mtu mmoja wa mji ule, mwenye pepo, hakuvaa nguo siku nyingi, wala hakukaa nyumbani, ila makaburini. Alipomwona Yesu alipiga kelele, akaanguka mbele yake, akasema kwa sauti kuu, Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu? Nakusihi usinitese. Kwa kuwa amemwamuru yule pepo mchafu amtoke mtu yule. Maana amepagawa naye mara nyingi, hata alilindwa kifungoni na kufungwa minyororo na pingu; akavikata vile vifungo, akakimbizwa jangwani kwa nguvu za yule pepo. Yesu akamwuliza, Jina lako nani? Akasema, Jina langu ni Jeshi; kwa sababu pepo wengi wamemwingia. Wakamsihi asiwaamuru watoke kwenda shimoni. Basi, hapo palikuwa na kundi la nguruwe wengi wakilisha mlimani; wakamsihi awape ruhusa kuwaingia wale. Akawapa ruhusa. Pepo wakamtoka mtu yule wakawaingia nguruwe, nalo kundi lilitelemka gengeni kwa kasi, wakaingia ziwani, wakafa maji. Wachungaji walipoona lililotokea walikimbia, wakaieneza habari mjini na mashambani. Watu wakatoka kwenda kuliona lililotokea, wakamwendea Yesu, wakamwona mtu yule aliyetokwa na pepo ameketi miguuni pa Yesu, amevaa nguo, ana akili zake; wakaogopa. Na wale waliokuwa wameona waliwaeleza jinsi alivyoponywa yule aliyepagawa na pepo. Na jamii ya watu wa nchi ya Wagerasi iliyo kando kando walimwomba aondoke kwao, kwa kuwa walishikwa na hofu nyingi; basi akapanda chomboni, akarudi. Na mtu yule aliyetokwa na pepo alimwomba ruhusa afuatane naye; lakini yeye alimwaga akisema, Rudi nyumbani kwako, ukahubiri yalivyo makuu Mungu aliyokutendea. Akaenda zake, akihubiri katika mji wote, yalivyo makuu mambo aliyotendewa na Yesu.” Tunataka kuangalia hiki kikwazo cha akili kufungwa katika malengo ya maisha ya mtu. Tunamwona huyu mtu akili zake zilifungwa ingawa mapepo yalikuwa mengi sana juu yake lakini mapepo hayo yalilenga kushika na kufunga akili zake ili zisifanye kazi inayotakiwa na aliishi kama mtu asiye na akili kabisa . Ili tuliangalie hiki kikwazo kuna mambo kadhaa tunapaswa tufahamu kwa undani kuhusu akili ili upate kuelewa kama umekwama hapo Mungu aweze kukufungua. JAMBO LA KWANZA. MTU NI ROHO, ANAYO NAFSI ANAKAA NDANI YA MWILI. 2 Wakorintho 7:1 “Basi, wapenzi wangu, kwa kuwa tuna ahadi hizo, na tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa mwili na roho, huku tukitimiza utakatifu katika kumcha Mungu.” Nataka tuone vitu vitatu hapo yaani NAFSI, ROHO NA MWILI. Ukisoma pia Zaburi 42:5 “Nafsi yangu, kwa nini kuinama, Na kufadhaika ndani yangu? Umtumaini Mungu; Kwa maana nitakuja kumsifu, Aliye afya ya uso wangu, Na Mungu wangu.” Hapo anayesema “Nafsi yangu…” ni roho ya Daudi kwamba inataka kutuambia inayo nafsi na hiyo nafsi inakaa ndani yake. Kwa hiyo mtu ki roho anayo nafsi na anakaa ndani ya mwili. JAMBO LA PILI 2. ROHO YA MTU ILIUMBWA KWANZA HALAFU UKAUMBWA MWILI NDIPO NAFSI IKAUMBWA. Mwanzo 2:7 “BWANA Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.” Mwanzo 1:27 “Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba.” Sura ya pili inatuambia hakukuwa na mtu wa kuilima ardhi kwa hiyo Mungu hakuinyeshea mvua ardhi. Sura ya kwanza inasema Mungu alimuumba mtu kwa mfano wake mwanamume na mwanamke aliwaumba. Lazima uzisome hizi sura mbili kwa pamoja kila sura kwa wakati mmoja maana ukisoma moja moja zitakusumbua kwenye uumbaji. Maana ukitaka kufahamu jinsi uumbaji ulivyoenda sawa ni lazima usome hizi sura zote mbili kwa pamoja maana zinaenda pamoja Sura ya kwanza Mungu alimuumba mtu roho, yaani roho yake ndipo ilipoumbwa, aliumba kwa mfano wake mwanamume na mwanamke wote roho zao ziliumbwa sura ya kwanza. Sura ya pili unaona vitu vyote vilivyokuwa vikitamkwa kwenye sura ya kwanza huvioni. Hakukuwa na mche wowote kondeni wakati kule mwanzo kulikuwa na miti na kila kitu vizae na alizungumza juu ya wanyama, ndege na n.k lakini kwenye sura ya pili huvioni unaona vyote vinatoka kwenye udongo. Alikuwa anatengeneza miili yao. Maana mtu alipoumbwa mwanzoni walipewa mwili mmoja mwanamume na mwanamke waliishi kwenye mwili mmoja.

    10 min
  2. EPISODE 2

    Nafsi na mwili viliumbwa vimilikiwe na roho

    NAFSI NA MWILI VILIUMBWA VIMILIKIWE NA ROHO Zaburi 63:1 “Ee MUNGU, Mungu wangu, nitakutafuta mapema, Nafsi yangu inakuonea kiu, Mwili wangu wakuonea shauku, Katika nchi kame na uchovu, isiyo na maji.” Mwandishi anamwambia Mungu, “Mungu wangu nitakutafuta mapema”, anaposema nitakutafuta ni roho ya Daudi inamweleza Mungu ya kwamba nitakutafuta mapema. Roho hiyo hiyo inasema kwa niaba ya nafsi, inasema nafsi yangu inakuonea kiu, lakini pia inasema kwa niaba ya mwili inasema mwili wangu wakuonea shauku. Nilitaka uone ya kwamba hauwezi kusema nafsi yangu kama haijapangiwa imilikiwe na roho na hauwezi kusema mwili wangu kama roho haikupangiwa kumiliki mwili. Ni dhambi iliyokuja na kukorofisha utaratibu wa uumbaji na mwili ukaonekana kama ndio unao tawala kila kitu, lakini Mungu aliweka kwa makusudi kabisa kwamba roho ya mtu ndiyo imiliki nafsi na mwili. AKILI IMO NDANI YA NAFSI Ayubu 32:8 “Lakini imo roho ndani ya mwanadamu, Na pumzi za Mwenyezi huwapa akili.” Unganisha na kile kitabu cha Mwanzo ili uelewe vizuri zaidi: Mwanzo 2:7 “Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.” Kwa hiyo kama pumzi iliachilia nafsi ndani ya mtu na pumzi iliachilia akili ndani ya mtu kwa hiyo akili imo ndani ya nafsi. Akili tumeipata kwa msaada wa pumzi ya Mungu na nafsi tumeipata kwa msaada wa pumzi ya Mungu. Wakati nafsi inaingizwa ndani yetu na akili ziliingizwa, na ndiyo maana kama unayo nafsi lazima na akili unazo, hakuna mtu ambaye ameumbwa bila akili, ile kwamba huzitumii haina maana kwamba huna. AKILI SIO UBONGO, LAKINI MUNGU ALIVIUMBA VIFANYE KAZI KWA KUSHIRIKIANA Biblia ya Kiswahili inafundisha vizuri zaidi juu ya akili kuliko Biblia ya Kiingereza. Ukisoma Biblia ya Kiingereza unahitaji kuwa mwangalifu sana kutafuta neno akili kwa sababu limeandikwa kwa tafsiri tofauti tofauti kutegemeana na waliokuwa wakitafsiri na inategemea pia picha nzima ya habari inayozungumzwa. Kwa sababu ubongo kwenye Kiingereza wanasema ni Brain lakini wengine wanasema ni Brains wengine wanasema ni intelligence na wengine wanasema ni mind lakini kwenye Biblia ya Kiswahili wamenyooka na kupata neno nzuri kabisa ambalo ni akili. Ubongo upo kwenye mwili na akili ipo kwenye nafsi. Na ndiyo maana hata ukienda hospitali wataalam watakuambia ubongo ulipo lakini watapata shida sana kukueleza akili zilipo. Mungu aliumba akili na ubongo vifanye kazi pamoja lakini akili imo ndani ya nafsi na ubongo umo ndani ya mwili. Kazi ya ubongo ni kupokea elimu na kazi ya akili ni kuchukua elimu na kuibadilisha kuwa maarifa Ubongo haubadilishagi elimu kuwa maarifa. Na ndiyo maana ukishikwa akili zako hata kama una akili kiasi gani ubongo unaweza kukusaidia ukafaulu darasani lakini huwezi kufaulu kwenye maisha. Kwa sababu maisha hayafaulishwi na ubongo wako bali ufaulishwa na akili yako na nafsi yako. Biblia inasema watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa na sio kwa kukosa ubongo. Na ndiyo maana mtu anaweza kuwa na shahada kadhaa lakini maisha hana. Ile tu kwamba mtu amesoma haina maana kisomo kinampa maisha. Kisomo kinaweza kikakupa cheti, kazi, heshima kwenye jamii lakini hakiwezi kikakupa maisha kwa sababu maisha yalinyang’anywa dhambi ilipoingia maana mwanadamu hakupewa maisha ya kwake alipewa maisha ya Mungu ambayo yanaitwa uzima. Yesu alisema nimekuja ili wawe na uzima kisha wawe nao tele. Huwezi kupata maisha ambayo Mungu aliyakusudia nje ya Yesu. Ubongo unapokea habari/information lakini akili inageuza habari kuwa ufahamu Haisemi ndipo akawafunulia akili zao wapate kusoma maandiko, kusoma hakuna shida, unaweza kusoma Biblia, ukakariri na kuimaliza yote lakini kuielewa akili lazima iingie kazini.

    10 min
  3. EPISODE 3

    Unapookoka neno la mungu huanza kushughulikia akili zako

    1 Petro 2:1-2 “Basi, wekeni mbali uovu wote na hila yote, na unafiki na husuda na masingizio yote. Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu;” Hakusema maziwa ya Roho amesema maziwa ya akili, Neno la Mungu unalopewa unapookoka mahali pa kushughulika napo pa kwanza ni akili zako ili upate kuukulia wokovu, ndio maana akili zikibanwa haijalishi umeokoka miaka mingapi huwezi kukua kiroho, ndio maana huwezi kujivunia miaka uliyokaa ndani ya wokovu, Mungu anaangalia umekua kiasi gani na usipojua kwamba Mungu kaziweka akili kwa makusudi kabisa macho na ubongo vitakusaidia kusoma Biblia lakini haviwezi vikakusaidia kuelewa. Mathayo 7:24 “Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba;mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba. Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa.” Huyu ni Yesu anazungumza anasema mtendaji wa Neno amefaninishwa na mtu mwenye akili hajasema amefananishwa na wa kiroho. Watu wengi sana hawajui namna ya kuunganisha akili na imani, wanafikiri mtu aliyeokoka akitumia akili anaenda kimwili na sasa umeelewa kwamba akili haziko kwenye mwili, Biblia imekataza tusizitegemee akili lakini tuzitumie akili. Yule mtu ambaye alikuwa na kichaa alipofunguliwa yale mapepo wale watu kwenye kijiji walikuja kumtazama pamoja nakumwona amevaa nguo na ana utulivu wakagundua ana akili zake. Maana yake walitambua ya kwamba huyu mtu maisha aliyokuwa anaishi akili hazikuwa kazini. Ukisoma hiyo mistari vizuri kwa jicho la mwalimu kuna kitu hapo utaona Luka 8:22,37 “Ikawa siku zile mojawapo alipanda chomboni yeye na wanafunzi wake, akawaambia, Na tuvuke mpaka ng’ambo ya ziwa. Wakatweka matanga. Na jamii ya watu wa nchi ya Wagerasi iliyo kando kando walimwomba aondoke kwao, kwa kuwa walishikwa na hofu nyingi; basi akapanda chomboni, akarudi.” Roho Mtakatifu alimbana Yesu wakati huduma ilikuwa inaendelea ukitazama pale aliporudi mkutano ulimkaribisha kwa furaha kwa maana walimgojea wote utafikiri aliwaambia kuna jambo naenda kuangalia narudi sasa hivi, maana aliporudi tena ng’ambo mkutano mkubwa ulikuwa unamgojea. Yule mtu Biblia haituambii jina lake lakini mbingu zilikuwa zinamfahamu na maandiko yanatuambia alikuwa na kwao kwa sababu alipotaka kumfuata akamwambia nenda rudi nyumbani kwako. Inawezekana alikuwa na wazazi, alikuwa na ndugu alikuwa na majirani, alikuwa pia na marafiki lakini mazingira yalimbana kiasi kwamba akawa anashinda makaburini na milimani na maandiko yanasema kuna kipindi ilibidi afungwe ili kuweza kuhimili ile vurugu ambayo alikuwa anafanya. Inawezekana wote walimkatia tamaa na yale mapepo yalikuwa ndani ya mtu na yalikuwa yanamkwamisha yeye mwenyewe maana anakimbilia kufanya vitu na yanamkwamisha. Maana tunaona mapepo baada ya kutoka yaliingia ndani ya nguruwe na kuwapeleka majini kwa kasi. Sasa haya mapepo ndio yalikuwa ndani ya mtu yakimsukumia wazo la kufanya na kinamharibu na kumwamisha jumla kabisa. Hii unaweza ukasikia mtu akisema “nimemlea huyu mtoto nikifikiri akili anazo kumbe hana”. Ukishasikia lugha ya nmna hiyo ina maana akili hazifanyi kazi inayotakiwa kwa sababu hamna mtu ambaye hana akili ila kuna namna zimebanwa.

    10 min
  4. EPISODE 4

    Uko mahali kwenye maisha yako kila kitu kimesimama, Yesu anakutafuta

    Hii unaweza ukasikia mtu akisema “nimemlea huyu mtoto nikifikiri akili anazo kumbe hana”. Ukishasikia lugha ya nmna hiyo ina maana akili hazifanyi kazi inayotakiwa kwa sababu hamna mtu ambaye hana akili ila kuna namna zimebanwa. Sasa angalia yule kijana wa nchi ya Wagerasi kila mtu alikuwa kamkatia tamaa. Sasa Yesu alikuwa hafanyi jambo lolote isipokuwa kamuomba baba akifanya. Kwa hiyo walikuwa anafanya mapenzi yake maana alikuwa akimuona Yesu kayakamilisha. Yesu aliposema tuvuke mpaka ng’ambo ina maana aliuacha mkutano mkubwa alafu akaingia katika boti kwenda ng’ambo mpaka nchi ya Wagerasi. Wanafunzi wake walikuwa hawajui wanaenda kufanya nini huko lakini Roho Mtakatifu alikuwa anajua kwamba kuna mtu yupo makaburini hapati hata msaada maana tunaona hakupelekwa na watu kwa Yesu. Maandiko yanatuambia kuwa Yesu alipofika tu alianza kukemea mapepo na ndio maana yalianza kupiga kelele kuwa tuna nini na wewe Yesu. Yesu alimfuatilia yule kijana maana tunaona hamna mtu aliyempeleka kwa Yesu kwa sababu kulikuwa na mkutano ng’ambo ya ziwa kwa sababu wangekuwa na haja ya kumpeleka wangempeleka kwa Yesu alipokuwa ng’ambo maana boti zilikuwepo za kuweza kuwavusha hata ng’ambo ya pili. Kila mtu alikuwa amemuacha na hapati msaada hata ndugu zake hawakumsaidia. Unisikilize inawezekana kabisa uko mahali na kila kitu chako kimekwama, nipo hapa kukuambia neno la Bwana kuwa Yesu yupo ng’ambo na atakuja kukufuata na wewe ili aje kukutembelea. Haijalishi maisha yako yako mahali pagumu kiasi gani kama vile makaburini Yesu atakuja yeye mwenyewe kukufuata hata kama haujakaribishwa kwenye mkutano. Yesu alipomfuata yule kijana alihusika moja kwa moja na akili zake maana alijua kabisa ya kwamba yule kijana akifunguliwa akili tu anaweza akasimama peke yake. Yule kijana alipoponywa biblia inatuambia alivaa nguo. Sasa swali linakuja hizo nguo alizipata wapi? Kwa hiyo inawezekana kabisa hakuchana nguo zote bali alikuwa anavua kila akivalishwa. Maana hatuoni kama kuna mtu alimpa nguo hata watu wa pale maana hata Yesu mwenyewe hakuja na nguo wala wanafunzi wake za kumpa yule kijana. Biblia inatuambia kuwa wanakijiji walipokuja walimkuta tayari kavaa nguo. Wafugaji wa pale walioopona nguruwe wamejimwaga baharini walikimbia mtaani kuwaeleza watu. Sasa yule kijana akili zake ziliporudi alitafuta nguo zake. Sasa akili zikifanya kazi jamii itakupa heshima hata kama haitaki. Biblia inatuambia kuwa walipokuja walimkuta yule kijana aliyekuwa na pepo kavaa nguo zake na katulia pale na akili zake zikiwa vizuri waliogopa sana. Baada ya hapo walimuomba Yesu aondoke kwao, na Yesu alitii aliondoka akapanda boti na akarudi kwenye mkutano. Mungu anaweza akaleta semina hii kwa ajili yako tu. Kwa hiyo isikusumbue umati wa watu bali angalia kama Yesu amekutembelea au hajakutembelea. Kuna watu kwenye biblia tunaona watu waliokuwa wanaleta wagonjwa kwa Yesu ili wapate msaada lakini yule kijana wa nchi ya Wagerasi hakuna aliyempeleka kwa Yesu. Labda inawezekana watu walimuogopa kwa sababu alikuwa mgomvi na ana mapepo. Sasa inawezekana kuna mtu wa namna hiyo nyumbani kwenu ambaye mnasema mtu huyu anakua mwili tu ila akili hamna na mnamkalia na kikao kabisa kwa ajili yake maana mna wasi wasi na akili zake. Kuna watu wengi sana ambao shetani kabana akili zao na za ndugu zao maana shetani hafungi mwili tu bali anafunga na akili pia. Shetani anaweza akalenga kufunga akili zenyewe kwa sababu ya umuhimu wake kwa sababu atakuwa ameshika sehemu kubwa sana ya akili yake na anakwamisha maisha yake. Kuna mtu unakuta kasoma vizuri sana na ana degree mbili hivi au tatu. Anaanza kazi vizuri kabisa lakini baada ya muda anaacha. Ukimwuliza kwanini atakuambia kuwa huku kazini wananisumbua sumbua tu. Sasa unamwuliza sasa utafanya nini sasa anasema nitafanya biashara. Hapo mtaji hana, hana hata uzoefu wa biashara, kakaa tu hapo nyumbani ila anasema nitafanya biashara. Baada ya hapo utamuona anaanza kuingia kwenye vijiwe na kukaa na watu huko. Hii ni kwa sababu akili zinafanana na anao kaa nao maana akili huwa zinaitana. Biblia inasema aonavyo nafsini mwake ndivyo alivyo. Kwa hiyo kama unataka kubadili maisha yako tazama wanaokuzunguka. Kwa sababu kama wanafanana na wewe katika kufikiri. Kama unawapenda sana kaa nao mbali kwanza alafu alafu ukikaa sawa ndipo uje uwatoe kama gari iliyokwama kwenye matope. Maana hamuwezi kusaidiana wote mkiwa kwenye matope, Ondoka kwanza kwenye kijiwe katafute msaada kwa Yesu, na ukirudi ukiwa umebadikika ndipo uje uwatoe kwenye kijiwe. Kwa sababu wataona namna kufikiri kwako na kuwaza kwako kulivyobadilika kwa sababu kuna kitu Mungu amefanya kwenye akili zako na zimefunguliwa.

    10 min
  5. EPISODE 6

    Akili za mwanadamu zingekuwaje kama tusingepitia dhambi, ungekuwa wapi sasa?

    Jana tuliangalia kikwazo cha kwanza ni AKILI KUFUNGWA NA SHETANI na tukaangalia kwenye kile kitabu cha Luka 8:26 - 39 tukaangalia kwa undani pamoja na mistari mingine na maelezo kwa undani. Saa nyingine huwa nawaza sana namna akili ya mwanadamu ilivyo na ambavyo inafanya mambo makubwa je kama tusingepita kwenye dhambi ingekuwaje? Kwa sababu vitu vingi vimebuniwa na akili ya mwanadamu ambayo iko kwenye dhambi na ina kiwango cha kufanya kitu ilichokifanya, sasa fikiria kama asingekuwa na dhambi ingefanya vikubwa kiasi gani? Sijasoma kwenye Biblia, lakini najaribu kufikiria kuwa kama tukifika mbinguni halafu Mungu atatuonyesha tumetumia kiwango gani cha akili zetu alizotupa na tukajikuta tumetumia kiasi kidogo sana mfano ¼, au 5% au 10% na asilimia iliyobaki akatuonyesha kulikuwa na kitu gani .Pia hiyo akili ambayo haijatumika je tungeitumia tungekuwa na maisha ya aina gani. Nakuambia watu wengi wangekata rufaa ya kurudi duniani kwa sababu ndani yake wangegundua kuwa kuna vitu vikubwa sana. Tukiangalia mfano wa Yusufu mtoto wa mzee Yakobo kwenye Mwanzo 41, aliitwa ofisini kwa Farao kutafsiri ndoto ya Farao aliyoiota usiku na kurudia mara mbili. Mara ya kwanza Farao aliota ng'ombe wanono saba halafu wakaja wengine waliokonda kutoka kwenye mto. Wale waliokonda wakawala wale wenye afya na hata baada ya kuwala wakabaki wamekonda vile vile, akaamka; akalala na kuota ndoto nyingine akaona masuke na asubuhi yake akatafuta msaada wa tafsiri kila kona kwa waganga, wachawi na wenye hekima ili wamsaidie. Mpaka mfanyakazi wake akaeleza alivyokutana na Yusufu jela na namna alivyo weza kuwatafsiria ndoto zao. Baada ya kusikia habari ya Yusufu ndipo Farao akaagizwa Yusufu aitwe mbele zake.Yusufu alipopewa taarifa za kuitwa kwa Farao tunona akamtafsiria Farao ndoto zake na kumweleza juu ya ujio wa miaka 7 ya chakula na unono. Baada ya pale Farao akata kujua zaidi miaka 7 ya njaa. Aliambiwa hiyo njaa itakuwa kubwa mno kiasi ambacho miaka 7 ya unono itaonekana kama haikuwepo ndio maana aliona ng'ombe waliokonda wakiwala walionona. Baada ya kuwala wale ng’ombe , wale waliokonda hawakunenepa ili kuonyesha kuwa kipindi cha njaa kitakuwa kibaya sana. Yusufu alipomaliza kumtafsiria Farao ndoto alimwelezea kitu cha kufanya kwa sababu alikuwa anajiandaa kurudi jela. Alimwambia Farao “tafuta mtu mwenye akili na hekima umweke kwenye nafasi afanye yafuatayo

    10 min
  6. EPISODE 7

    Haijalishi unapitia hali gani na upo kwenye kipindi gani, Mungu yuko pamoja nawe

    Mtu aliyekuwa anatakiwa kwenye hii nafasi alitakiwa awe ana akili ya miaka 14 kusaidia Misri na nchi za jirani. Alitakiwa awe ana hekima pamoja na Roho wa Mungu ili kuweza kukamilisha jukumu hilo. Yusufu aligundua kuna kitu Farao alitakiwa akitolee nafasi (position) kwa sababu anaweza patikana mtu mwenye akili lakini asiwe na mahali pa kutumia akili zake. Kuna watu wana akili lakini hawana hekima na wengine wana hekima akili hawana. Yusufu alikuwa na hivyo vyote pia alikuwa na Roho wa Mungu ndani yake. Kwa maana hiyo Mungu alimpa nafasi ili aweze tumia akili, hekima na Roho ya Mungu iliyokuwa ndani yake katika kufanya alichotakiwa kufanya kwa miaka 14. Mwanzoni kabisa Yusufu aliotea ndoto akiwa na miaka 17 lakini alipewa kuwa waziri mkuu akiwa na miaka 30, kwa hiyo miaka 13 ilimtesa kufukia mahali pa kuweza kutumika miaka 14. Kwa sababu alipitia wakati mgumu sana miaka hiyo 13 maana Mungu alimleta duniani kwa kazi hizo kubwa. Moja ya kazi ni kuhakikisha ile miaka 14 pale Misri akili zake zinatumika sawasawa kwa sababu alisema Mwanzo 45:7‭-‬8 “Mungu alinipeleka mbele yenu kuwahifadhia masazo katika nchi, na kuwaokoa ninyi kwa wokovu mkuu. Basi si ninyi mlionipeleka huku, ila Mungu; naye ameniweka kama baba kwa Farao, na bwana katika nyumba yake yote, na mtawala katika nchi yote ya Misri.” Maana yake amekuwa na akili iliyomfanya kuwa baba kwa Farao mahali ambapo kwa jinsi ya kawaida isingewezekana pia akawa baba kwa taifa la Misri na kwa ndugu zake. Yusufu ndoto (vision) yake ilikuwa ya contract ya miaka 14. Lakini alifanya vizuri kiasi ambacho hakustaafishwa baada ya muda wake kuisha bali aliendelea na kazi mpaka alipo kufa. Kumbuka Yusufu alipewa akili ya kusaidia ndugu zake lakini ndugu zake walimkataa hata alipoenda kuwapelekea chakula walipomwona walimkasirikia wakaanza kupanga kumu ua. Sasa fikiria walitaka kuua akili ya namna gani kwa kubebeshwa kitu cha aina gani. Kwa hiyo ili wasimuue wakakubaliana kumtumbukiza kwenye kisima kisicho na maji halafu wakafikiria tena kuwa wamuuze kama mtumwa bila kujua thamani ya akili iliyokuwa inauzwa. Waishmaeli nao wakaja kumuuza kwa Potifa na Potifa baadae akamtazama akagundua Yusufu ana baraka fulani na sio akili tu. Potifa akamweka Yusufu kuwa kiongozi wa kila kitu nyumbani kwake. Aliposhindwana na mke wa Potifa akaishia jela, sasa fikiria ni akili gani ambayo ilikuwa imefungwa jela. Kuna wengine wamefungwa jela (jela hizi za kawaida kwa makosa halali au kwa kusingiziwa/kuonewa) na wana akili kama ya Yusufu. Pia mkuu wa jela akagundua baraka zilizokuwa juu ya Yusufu na kumpa cheo. Naye Yusufu akamsaidia mtu mkubwa sana katika taifa la Misri kwa kumtafsiria ndoto yake na akamwambia akirudi kazini kwake amkumbuke ili aweze toka jela. Lakini yule mtu alimsahau kwa hiyo Yusufu alisahauliwa jela miaka miwili. Ninaposoma hizi habari huwa namshangaa sana Mungu. Inawezekana umesahauliwa huna nafasi yoyote, huna kazi lakini hujui akili uliyobeba na inawezekana hata waliokuzunguka hawajui akili uliyobeba.Maana unaweza ukawa na upako lakini kuna watu wanaojaribu kutafuta kukuua na Mungu amenyamaza. Unaweza ukawa ndani ya birika na ndugu zako wakakuchukia kabisa. Usije ukafikiri Mungu amekuacha maana nguvu za Mungu ziko pamoja na wewe. Inawezekana unaishi maisha kama ya kitumwa lakini mkono wa Bwana uko pamoja na wewe. Yusufu alikuwa na Mungu kwenye kila mazingira toka anauzwa, alipopelekwa mahakamani kwa sababu ya mke wa Potifa Mungu alikuwa pamija nae. Alipokuwa jela alikuwa pamoja na Mungu kwa hiyo kila sehemu Mungu alikuwa pamoja nae. Kwa hiyo usije ukafikiri waliofungwa jela hawana Mungu wako pamoja na Bwana. Shetani alikuwa anagombana na akili za Yusufu ili zisipate nafasi ya kutumika maana alikuwa ana akili ya kusaidia familia yake lakini alinyimwa heshima nyumbani kwake. Akili alilozokuwa nazo Yusufu zilikuwa na uwezo wa kumsaidia baba yake lakini aliondolewa nyumbani kwao na kukatiwa mawasailiano na baba yake ili ajue kwamba amekufa. Shetani alikuwa akiwinda baba yake yaani mzee Yakobo asipate msaada wa akili za Yusufu. Unaweza ukawa unafurahia biashara uliyonayo na kufikiri kwamba umefika lakini Mungu ana kitu kikubwa kuliko unachofikiri. Ila hujajua kwamba huko ndani yako kuna kitu gani kimekaa na kwanini ndani yako unaona ndoto kubwa au unaona hujaridhika mahali ulipo kumbe Mungu anajaribu kukusukuma kukuonyesha kwamba ndani yako amekuwekea kitu kikubwa kuliko unacho fikiri. Hivyo usitosheke na mahali ulipo kisukume na usonge mbele na ukimwendea Mungu atakuonesha mahali unapotakiwa kuwa. Mungu alimpa Yusufu miaka 14 ya kutumia zile akili. Na ndiyo maana si suala la kuishi maisha marefu ni suala la kuishi katika mapenzi ya Mungu.

    10 min
  7. EPISODE 8

    Sio swala la kuishi maisha marefu, ni swala la kuishi kwenye mapenzi ya Mungu

    Unaweza ukawa unafurahia biashara uliyonayo na kufikiri kwamba umefika lakini Mungu ana kitu kikubwa kuliko unachofikiri. Ila hujajua kwamba huko ndani yako kuna kitu gani kimekaa na kwanini ndani yako unaona ndoto kubwa au unaona hujaridhika mahali ulipo kumbe Mungu anajaribu kukusukuma kukuonyesha kwamba ndani yako amekuwekea kitu kikubwa kuliko unacho fikiri. Hivyo usitosheke na mahali ulipo kisukume na usonge mbele na ukimwendea Mungu atakuonesha mahali unapotakiwa kuwa. Mungu alimpa Yusufu miaka 14 ya kutumia zile akili. Na ndiyo maana si suala la kuishi maisha marefu ni suala la kuishi katika mapenzi ya Mungu. Kuna wengine wanaishi maisha marefu na maisha yao hutaki hata kuyasikia, maana ni hasara tu mpaka kwa udongo. Lakini kuna wengine wana maisha mafupi kama ya Yesu, maana yeye alikufa kabla ya kufikisha miaka 40 na ni miaka 3 ndiyo iliyomleta hapa duniani miaka mingine unaona wakiandika habari zake kwa uchache sana. Miaka yake 3 ilibadilisha kila kitu na kuweka alama ambayo shetani hawezi kufuta. Sijajua Mungu amekupa mtu wa namna gani, au kwamba Mungu amekubebesha akili za namna gani ila ninachojua akina Yusufu wako tena yawezekana ni wewe. Wakati ukifika haijalishi uko jela au umesingiziwa Mungu atakutoa tu huko, ikifika saa ya kwako Mungu atatengeneza njia tu hata kama hakuna njia na kukufikisha mahali kila mtu atakutazama na kusema kama si Mungu aliyekuwa pamoja naye huyu mtu na aseme sasa. Na ndiyo maana Yusufu pamoja na kulia alipowaona ndugu zake hakuwa na sababu ya kuwachukia na kuwakasirikia alijua ya kwamba kama si Mungu wasinge fika pale na yeye asingefika pale. Kwa hiyo ukiona watu wanakuchukia na kukupiga vita njiani wakati unasonga mbele huhitaji kuwakasirikia wewe songa mbele maana hao hao wanaokuchukia leo kesho watakuja kukuomba mkate. Kwa hiyo ukiwa na akili kubwa usishindane na vidogo. Usiwe na muda wa kupoteza kwenye vitu ambavyo vinakuletea hasara tu. Nilikuambia akili sio ubongo akili iko ndani ya nafsi na ubongo uko ndani ya mwili lakini Mungu aliviumba vifanye kazi kwa pamoja kwa kushirikiana.

    10 min

Trailer

Ratings & Reviews

About

Ni salama rohoni mwangu ni Podcast inayokusaidia kuboresha mahusiano yako na Mungu kupitia mafundisho mbalimbali yanayotolewa na wahubiri, walimu na wachungaji kiganjani mwako. Tunakusaidia kuweza kuanza siku vyema ukiwa na neno la mungu kama taa itakayokuwa ikikuongoza katika shughuli zako za kila siku. Kupitia Ni Salama tutakuletea mafunzo na masomo yatakayokuwezesha kuelewa zaidi neno la Mungu linalopatikana kwenye Biblia huku tukikuongezea hamu na mvuto wa kuisoma Biblia yako. Karibu